Oct 31, 2013

Apigwa Risasi Baada Ya Kutishia Kwa Bastola

ASKARI Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Vurugu (FFU), amempiga risasi ya bega mwanamke, Vaileth Mathias ambaye anadaiwa alitishia kuwapiga risasi polisi kwa bastola yake.

Mwanamke huyo anadaiwa kukaidi amri ya polisi ya kumtaka asiegeshe gari lake kwenye eneo la lango la kuingilila benki na ofisi za TRA Arusha, na hivyo polisi waliamua kulitoa upepo.

Baada ya mwanamke huyo kutoka ndani ya benki na kukuta gari lake lenye namba za usajili T 888 BWW limetolewa upepo kwenye magurudumu, alikasirika na kutoa bastola huku akiwafuata askari, ndipo katika kujihami mmoja wao alimpiga risasi ya bega la kushoto.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana saa 7:00 mchana eneo la CRDB Mapato lililopo mkabala na Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani Arusha.

Kamanda Sabas alisema kuwa tukio hilo limetokea baada ya mwanamke huyo kukaidi amri ya polisi waliokuwa wakilinda benki hiyo ya kumtaka asiegeshe gari hilo eneo hilo.

Alisema kwa hasira mwanamke huyo alimfuata polisi aliyekuwa kwenye lindo na kumwambia hata kama ana bastola naye pia anayo.

Kamanda alisema baada ya kutamka maneno hayo mwanamke huyo alitoa bastola na kutaka kumpiga askari huyo, lakini alimuwahi na kumpiga risasi kwenye bega la kushoto na hatimaye akaanguka chini.

Baada ya tukio hilo mwanamke huyo alikimbizwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu, lakini baadaye alihamishiwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) maarufu kwa jina la Selian.

0 comments:

Post a Comment