Sep 9, 2013

WAZIRI CHUPUCHUPU KUULIWA

Waziri wa mambo ya ndani wa Misri Mohamed Ibrahim amenusurika kuuawa katika mashambulizi ya bomu dhidi ya msafara wake, na kuonya kuwa taifa hilo linakabiliwa na wimbi jipya la ugaidi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Misri Mohamed Ibrahim amenusurika katika mashambulizi ya bomu dhidi ya msafara wake, na kuonya kuwa taifa hilo linakabiliwa na wimbi la ugaidi, huku kukiwa na ukandamizaji wa polisi dhidi ya wafuasi wa vyama vya Kiislamu.
Maafisa Usalama walisema bomu la kutegwa kwenye gari liliushambulia msafara wa waziri huyo majira ya saa nne na nusu asubuhi karibu na nyumbani kwake katika mji wa Nasr, katika shambulio la kwanza la aina hiyo mjini Cairo katika kipindi cha miaka kadhaa. Shambulio hilo ambalo limekuja wakati polisi ikiendelea na ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohammed Mursi, limezua hofu ya kurejea upya kwa uasi wa makundi ya wapiganaji wa Kiislamu ambao ulishuhudiwa nchini Misri katika miaka ya 1990.

Maafisa usalama wakikagua eneo lilikotokea shambulizi dhidi ya masafara wa Ibrahim.
 
Wizara ya mambo ya ndani ilisema msafara wa Ibrahim ulilengwa na bomu bila kutoa maelez zaidi. Afisa kutoka wizara ya afya alisema watu saba walijeruhiwa katika mripuko huo, wakati afisa mwingine wa waizara ya mambo ya ndani alisema maafisa wanne wa polisi walijeruhiwa, akiwemo mmoja aliepoteza mguu wake katika mripuko huo. Ibrahimi alijitokeza katika televisheni ya taifa saa chache baada ya shambulizi hilo na kulaani kile alichokiita jaribio la uoga la kutaka kumuua, akisema msafara wake ulilengwa na bomu ambalo liliwajeruhi walinzi wake wengi.

Ni mashambulizi yaliyotarajiwa
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa alionya juu ya vurugu za namna hiyo baada ya kuanza kwa ukandamizaji wa Agosti 14 dhidi ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu, ambao walikuwa wamepiga kambi mjini Cairo kupinga mapindizi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais Muhammad Mursi Julai 3. "Nilikuwa nimeonya kabla ya kutawanywa kwa migomo ya Rabaa na Nahda kwamba kutakuwa na wimbi la ugaidi. Hili lilitarajiwa," Ibrahim alisema.

Baraza la mawaziri liliahidi kuwashughulikia kwa mkono wa chuma, wale wote wanaotishia usalama wa taifa. Shirika la habari la Misri MENA liliripoti kuwa polisi ilifunga mara moja, njia zote zinazoelekea katika makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani katikati mwa mji wa Cairo baada ya mripuko huo. Mwandishi wa shirika la habari la AFP aliekuwepo katika eneo la tukio alisema magari kadhaa yaliharibiwa katika mripuko huo. Televisheni ya Taifa pia ilionyesha picha za jengo lililoharibiwa vibaya kwa mbele.

Muungano wa kupinga mapinduzi walaani
Muungano wa vyama vya Kiislamu unaoongozwa na Mursi ulilaani shambulio hilo. "Mashambulizi hayo ni ya kulaaniwa bila kujali wahusika ni kina nani," muungano huo ulisema ukiwanukuu wanachama wake waandamizi. Mamia ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi waliuliwa katika viwanja vya Rabaa al-Adaiya na Nahda, baada ya polisi kuvamia kambi za maandamano hayo Agosti 14.

Zaidi ya maafisa 100 wa polisi wameuliwa pia katika vurugu za wakati na baada ya ukandamizaji huo. Wafuasi wa rais Mursi wamesema wataendelea na maandamano ya amani, lakini wachambuzi wanasema wafuasi wa itikadi kali wanaweza kuanzisha uripuaji wa mabomu na mshambulizi. Jeshi na polisi tayari vinapambana na uasi katika rasi ya Sinai, mahala salama kwa wapiganaji sugu wanaohamasishwa na kundi la Al-Qaeda.
 
Siku ya Alhamisi wapiganaji walimuua afisa wa polisi katika rasi ya Sinai na kumpiga risasi mwanajeshi karibu na mji wa Ismailiya, uliko karibu na mfereji wa Suez, vilisema vyombo vya usalama. Mashambulizi pia yalifanyika katika miji yenye wakaazi wengi ya Nile Delta na Cairo. Raia wawili walijeruhiwa katika mripuko siku ya Jumatatu, baada ya washambuliaji kurusha bomu katika kituo cha polisi mjini Cairo.

Tarehe 24 Julai, afisawa polsi aliuawa wakati bimu liliporipuka katika kituo cha polisi katika mji wa Mansoura uliyopo jimboni Nile Delta. Misri ilikabiliwa na wimbi la mabomu na ufyatuaji risasi katika miaka ya 1990, ambavyo vilihusishwa na jaribio la uasi wa Waislamu wenye msimamo mkali, mashambulizi ambayo pia yalimlenga waziri wa mambo ya ndani katika jaribio la mauaji lililofeli.
 
 Gari lililoharibiwa katika mripuko huo.