Sep 9, 2013

RUTO MAHAKAMANI ICC



Naibu rais William Ruto anakabiliwa na mashtaka ya kuchocheza ghasia za baada ya uchaguzi Kenya
Naibu rais wa Kenya William Ruto, ameondoka kuelekea Hague Uholanzi ambako anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamau katika mahakama ya ICC. Kesi yake inatarajiwa kuanza siku ya Jumanne.

Maafisa wakuu wa serikali walimuaga Ruto katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.

Bwana Ruto na rais Uhuru Kenyatta, wameshtakiwa kwa kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu, ingawa wanakana kuhusika na mauaji yaliyotokea kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008.

Mnamo siku ya Jumapili, Rais Kenyatta alisema kuwa ICC lazima isikize kesi hizo kwa ratiba nzuri ambayo itawapa viongozi hao muda wa kurejea nyumbani kwani wote hawawezi kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja.
Kesi dhidi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi Novemba.

Mkuu wa kituo cha redio kilichodaiwa kuchochea mapigano katika mojawapo ya maeneo yaliyokumbwa na mapigano, Joshua arap Sang , ameshtakiwa kwa kosa la kuchochea mapighano na kusaidia watu kuyaandaa mapigano hayo.
Yeye pia amekanusha madai hayo.

Tuhuma dhidi ya wanaume hao watatu, yanatokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine laki sita kuachwa bila makao.

Kenyatta na Ruto walikuwa mahasimu wa kisiasa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007 na wanatuhumiwa kwa kupanga na kusaidia kutekeleza mapigano kati ya makabila hasimu.
Wadadisi wanasema kuwa kesi zao katika mahakama ya ICC ziliwasaidia katika kampeini zao kwani walizitumia kukosoa mataifa ya magharibi kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.

Mnamo siku ya Jumamosi, Kenyatta aliwakabidhi hundi ya zaidi ya dola elfu nne familia za watu ambao walilazimika kutoroka makwao kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu na ambao bado walikuwa wanaishi katika kambi za wakimbizi.

Wiki jana bunge la Kenya lilipitisha hoja ya mjadala wa Kenya kujiondoa katika mahakama ya ICC.