Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
amesifu hatua ya Misri kutaka kuleta miradi ya uwekezaji katika sekta
ya uvuvi wa bahari kuu visiwani Zanzibar, kwa vile sekta hiyo itatoa
fursa nyingi za ajira na kuinua uchumi wa serikali na wananchi.
Maalim Seif ameyasema hayo jana ofisini kwake Migombani mjini
Zanzibar, alipofanya mazungumzo na Balozi mdogo wa Misri Zanzibar,
Walid Mohammed Ismail.
Alisema Zanzibar ina utajiri mkubwa wa maliasili za baharini ambazo
hazijatumika ipasavyo kuinua uchumi na maisha ya Wazanzibari, hivyo
hatua ya kukaribisha uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni
muhimu kwa wakati huu.
Alisema iwapo miradi ya uvuvi inayokusudiwa kuanzishwa na kampuni za
Misri italeta mafanikio, wananchi wengi hasa vijana watanufaika na
ajira na hivyo kuondokana na ugumu wa maisha unaojitokeza.
Mapema, balozi huyo mdogo, alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa
mipango ya kuwawezesha wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu kuja
Zanzibar inaendelea na kwamba ujumbe kutoka Misri unatarajiwa kuwasili
mwezi ujao.
Balozi huyo alisema atawashawishi wawekezaji watakaofika Zanzibar
kuweka umuhimu mkubwa katika kufungua viwanda vya kusindika samaki na
mazao mengine ya baharini, ili kutoa fursa kubwa zaidi ya ajira kwa
wananchi.
|
0 comments:
Post a Comment