Sep 25, 2013

AL SHABBAAB yadai kuuwa Mateka 137



HAPA RAIS UHURU KENYATA AKILIHUTUBIA TAIFA NA KUTANGAZA KUMALIZIKA KWA MAPAMBANO KATI YA SERIKALI NA KUNDI LA AL SHABBAAB

Kundi la Al-Shabaab limedai siku ya Jumatano kuwa mateka 137 waliowachukua wamekufa katika uvamizi wa kituo cha biashara, idadi ambayo ni vigumu kuithibitisha na kubwa kuliko idadi iliyotangazwa kuwa hawajulikani walipo. 

Wapiganaji hao walio na mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, katika ujumbe waliouweka katika mtandao wa kijamii wa twitter, walisema mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa na mujahedeen walikufa. 

Waliwashtumu pia wanajeshi wa Kenya kwa kutumia vifaa vya kemikali kukomesha mkwamo huo uliodumu kwa siku nne. "Katika hatua ya uoga wa dhahiri, vikosi vya Kenya kwa maksudi vilitumia vilipuzi vilivyokuwa na kemikali," ulisema ujumbe mmoja na kuongeza kuwa, "ili kufunika uhalifu wao, serikali ya Kenya iliendesha zoezi la kuliporomosha jengo, na kuuzika ushahidi na mateka wote chini ya vifusi."

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alitangaza kumalizika kwa umwagaji huo wa damu uliodumu kwa saa 80 jioni ya Jumanne, ambao ulisababisha vifo vya raia 61 na maafisa sita wa vikosi vya usalama. 

Polisi ilisema idadi hiyo ya vifo ingeweza kuongezeka, ambapo shirika la misaada la Msalaba mwekundu liliorodhesha watu 63 ambao bado hawajulikani walipo. 

Hakukuwa na kauli kutoka serikali ya Kenya kuhusiana na madai hayo ya Al-Shabaab waliyoyatoa kupitia kwenye mtandao wa twitter.
Wanajeshi wa ulinzi wa Kenya wakijiandaa kuingia jengo la Westgate kupambana na wavamizi.  
Wanajeshi wa ulinzi wa Kenya wakijiandaa kuingia jengo la Westgate kupambana na wavamizi.
 
Kundi hilo lilisema lilifanya shambulizi hilo katika kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kutokana na kujiingiza nchini Somalia kupambana na wanamgambo hao. 

Katika moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika historia ya Kenya, wapiganaji hao waliingia katika jengo la maduka la Westagate lenye ghorofa nne, ambalo linamilikiwa kwa sehemu na raia wa Israel, mchana wa Jumamosi, na kuanza kuwashambulia wanunuzi kwa risasi na kuripua maguruneti.
 
Kenya ilianza siku tatu za maombolezi rasmi Jumatano, ambapo bendera za taifa zinapepea nusu mlingoti, huku wafanyakazi wa uokozi wakisafisha mabaki ya jengo la Westgate kutafuta miili ya wahanga wa tukio hilo. 

Karibu watu 200 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa siku nne, ambao ulishuhudia mapambano makali kati ya wapiganaji na vikosi vya usalama vya Kenya katika jengo hilo, ambalo ndicho kituo kikubwa zaidi cha biashara na maarufu kwa watu wenye uwezo nchini Kenya, wanadiplomasia, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na watalaamu wengine.

Picha kwa hisani kubwa ya Reuters.

0 comments:

Post a Comment