Aug 30, 2013

UNGA WAMNG'OA KAMANDA AIR PORT DAR.




Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema
BAADA ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kuwa njia kuu ya kusafirishia dawa za kulevya, hatimaye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema amemuondoa Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Deusdedit Kato.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mwema amemhamishia Kato makao makuu ya Polisi na nafasi hiyo inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Selemani Hamisi kutoka makao makuu Idara ya Upelelezi.

Kuondolewa kwa Kato, kunaelezwa na wachunguzi wa mambo kuwa kumetokana na kushindwa kudhibiti wimbi za mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwenye uwanja huo, huku askari polisi kadhaa wakishiriki kupitisha dawa za kulevya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na jeshi hilo mjini Dar es Salaam jana, ilisema Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Hamad Hamad ameteuliwa Mkuu wa Upelelezi Viwanja vya ndege, akichukua nafasi ya David Mwafwimbo aliyehamishiwa mkoani Lindi kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Lindi (OCD).

Katika mabadiliko hayo, IGP Mwema pia amemuondoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa ambaye amehamishiwa makao makuu ya Polisi Idara ya Upelelezi.

Katika mabadiliko hayo, nafasi ya Kamanda Sunzumwa inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Zelothe Stephen kutoka Makao Makuu ya Polisi.

Hatua ya IGP Mwema kumuondoa Kato, kumetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuwataja hadharani wafanyakazi wa uwanja wa ndege ambao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa kupitisha dawa za kulevya.

Waziri Mwakyembe, bila kuficha alisema mtandao wa wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya unazidi kuteketea, baada ya kuwafukuza kazi maofisa wanne ambao walikuwa zamu Julai 5, mwaka huu siku ambayo dawa za kulevya zilipitishwa kwenda Afrika Kusini.

Alisema kwa mujibu wa ushahidi wa picha za kamera za uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere, zimeonyesha wazi baadhi wa maofisa walivyoshiriki katika zoezi hilo. “Picha za kamera zinaonyesha mfanyakazi mmoja, Yusuph Daniel Issa akitoka nje ya jengo la abiria, akiingia ndani mara kadhaa huku akiongea na simu kitendo ambacho huwa hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa ukaguzi.”

Alisema wakati tukio hilo likiendelea, picha za kamera zimemuonyesha pia mfanyakazi mwingine Koplo Ernest akiwa anarandaranda eneo hilo hilo la ukaguzi wa pasipoti za abiria.

“Wizara inauagiza uongozi wa mamlaka za viwanja vya ndege kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wake wafuatao ambao walihusika kwa njia moja ama nyingine kupitisha mabegi tisa ya dawa za kulevya…Yusuph Daniel Issa, Chief Security Office, Jackson Manyoni, Chief security officer,” alisema Mwakyembe na kuagiza wafanyakazi hao kukamatwa mara moja
 

Inasemakana kuwa Uamuzi wa kuondolewa kwa Sunzumwa mkoani Mtwara, ni wazi kumechangiwa na wimbi la ghasia kubwa zilizotokea mapema mwaka huu.

Katika vurugu hizo, watu kadhaa na mali vilichomwa moto huku mamia ya wananchi wakikimbia makazi yao kuhofia kukamatwa.