Aug 16, 2014

MAREKANI UUA RAIA WAKE 400 KILA MWAKA

Ripoti zinaonesha kuwa, raia mia nne huuawa kila mwaka na polisi nchini Marekani suala ambalo linaonyesha ukatili mkubwa wa polisi ya nchi hiyo dhidi ya raia. 

Gazeti la Marekani la USA Today linaripoti kwamba, utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, kila mwaka raia mia nne huuawa na polisi nchini humo na kwamba, wengi wa wahanga hao ni jamii ya walio wachache. Aidha ripoti ya Shirika la Upelelezi la Marekani FBI inaonyesha kuwa, asilimia 18 ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wana umri wa chini ya miaka 21 wameuawa katika kipindi cha miaka saba iliyopita. 

Takwimu zinaonyesha kuwa, jamii za walio wachache nchini Marekani ni wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu vya polisi ya nchi hiyo. Wakati huo huo, malalamiko dhidi ya vitendo vya utumiaji mabavu vya polisi ya Marekani yameongezeka mno nchini humo.

 Leo kumeshuhudiwa maandamano katika miji kadhaa ya Marekani ikiwemo ya St. Louis na Ferguson. 

Polisi ya mji wa Ferguson hivi karibuni ilimuua kijana anayejulikana kwa jina la Michael Brown kwa kosa la kuiba pakti ya sigara yenye thamani ya dola 49. 

Hata hivyo wakili wa familia ya Michael Brown imekanusha vikali madai ya polisi na kusema hayana ukweli wowote; kwa maelezo kwamba Michael hakuhusika kabisa na wizi huo.

0 comments:

Post a Comment