Wakazi wa Kijiji cha Masusu, Kata ya Gisambalang wilayani
Hanang’ katika Mkoa wa Manyara wamepatwa na mshtuko kutokana na tukio
lenye utata la kuuawa mtoto Omary Hamis mwenye umri wa mitatu, kisha
mwili wake kutundikwa juu ya mti.
Inadaiwa kuwa Omary aliuawa na watoto wenzake
wawili ambao ni wakazi wa kijiji hicho kwa kumpiga kwa fimbo kisha
kumnyonga na baadaye kuutundika mwili wake juu ya mti.
Watoto wanaodaiwa kufanya kitendo hicho (majina
yao tunayahifadhi kwa sasa), mmoja ana umri wa miaka mitano na mwingine
miaka saba na wote wanashikiliwa na polisi katika Kituo cha Katesh,
mkoani Manyara kwa uchunguzi zaidi.
Diwani wa Kata ya Gisambalang, Masala Bajuta
alisema tukio hilo lilitokea Julai 26, mwaka huu saa 7 mchana na kwamba
watoto wanaodaiwa kufanya kitendo hicho walikuwa wakichunga mifugo ndipo
walipokutana na mtoto mwenzao.
Habari ambazo zilizotufikia kutoka
kijijini Masusu zinasema Omary ambaye ni mkazi wa Babati, alikuwa
amepelekwa kwa babu yake anayeishi kijijini hapo kwa ajili ya
kumsalimia, hivyo alikuwa mgeni katika eneo hilo.
Akiwa anacheza katika eneo linalozunguka nyumba ya
babu yake, Omary alitoweka na hakuonekana tena hadi pale taarifa za
mwili wake kukutwa umetundikwa kwenye mti zilipoifikia familia yake
ambayo wakati huo ilikuwa ikimtafuta.
Bajuta alisema siku ya tukio hilo Omary alipotea
njia na kukutana na watoto wenzake wawili waliokuwa wakichunga ng’ombe
na kuanza kumwongelesha Lugha ya Kidatoga ambayo haielewi kwa kuwa yeye
ni Mburunge kutoka Wilaya ya Babati.
“Baada ya kumuuliza jina lake kwa lugha yao na
yeye akawa haijui na kushindwa kujibu, watoto hao walianza kumpiga kwa
fimbo, wakamnyonga na kisha wakamtundika juu ya mti,” alisema Bajuta.
Alisema ndugu wa Omary walianza kumtafuta mtoto
huyo baada ya kutoonekana, na baada ya muda mama yake mkubwa alimuona
akiwa ametundikwa kwenye mti akiwa ameshafariki dunia.
Taarifa za ushiriki wa watoto hao katika tukio la
kuuawa Omary, zilitolewa na mtoto mwingine ambaye alishuhudia tukio
hilo. Mtoto huyo muda wote wakati marehemu akitafutwa, alikuwa kimya
lakini baadaye aliwaambia wazazi wake kwamba Omary ‘amekaa juu ya mti’.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit
Nsimeki alisema watoto hao wawili wanashikiliwa na polisi wakidaiwa
kumuua mtoto huyo.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili,
kwani ni jambo ambalo limetushangaza kutokana na mazingira ya kifo
chenyewe na umri wa watoto hao wawili wanaodaiwa kufanya mauaji hayo,”
alisema Kamanda Nsimeki.
0 comments:
Post a Comment