Jul 30, 2014

Watuhumiwa ugaidi waendelea kusota

Zanzibar. Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupilia maombi ya kutaka kuachiwa huru kwa watuhumiwa wanane wa ugaidi waliokamatwa Zanzibar na kufunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara.

Hoja ya maombi hayo ni kwamba mashkata hayo ni kinyume na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Mkusa Issack Sepetu baada ya kubainika makosa katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani na mawakili Rajab Abdallah Rajab na Abdallah Juma Mohamed wanaowatetea watuhumiwa hao.

Akitoa uamuzi wa kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya kamishna wa Jeshi la Polisi, Zanzibar, Hamdan Omar Makame na naibu mkurugenzi wa upelelezi na makosa ya jinai, Jaji Mkusa alisema maombi hayo yamekosa nguvu za kisheria baada ya kuwasilishwa kimakosa.

Alisema kwa mujibu wa sheria, hati ya kiapo baada ya kuwasilishwa mahakamani hutakiwa kusainiwa, kuonekana tarehe kabla ya kuorodheshwa katika kumbukumbu ya masjala, jambo ambalo halikuzingatiwa na mawakili.

Aidha, alisema makosa kama hayo pia yamefanywa katika hati ya kiapo kwa viongozi wa polisi waliokula kiapo baada ya kuonekana nyaraka zao zimewasilishwa kupitia mrajisi wa mahakama bila ya kuwa na terehe na siku waliokula kiapo.

Jaji Mkusa alisema kwa kuzingatia sababu hizo, mahakama imeona kuna upungufu wa kisheria katika hati ya kiapo kwa pande zote mbili na kuamua kutupilia mbali ombi hilo ambalo limefunguliwa na Mahakama Kuu wakipinga wateja wao kukamatwa Zanzibar na kufunguliwa kesi Tanzania Bara wakati kosa la shtaka ambalo wanatakiwa kujibu, lilifanyika visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, Jaji Mkusa alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa kifungu cha 93 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kimeeleza kuwa Zanzibar kutakuwa na mahakama zake na zitapewa nguvu za kisheria kusimamia kesi zote na kutambuliwa pia na ibara 214 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetambua kuwapo na kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment