Apr 17, 2014

Ufalme wa Saudia wamwondoa Prince Bandar kama mkuu wa kijasusi

 Prince Bandar bin Sultan akiwa katika kasri yake mjini Riyadh, Saudi Arabia, June 4, 2008.
Prince Bandar bin Sultan akiwa katika kasri yake mjini Riyadh, Saudi Arabia, June 4, 2008.

Mkuu wa idara ya kijasusi ya Saudi Arabia, Prince Bandar Bin Sultan, ameondolewa kutoka wadhifa huo kufuatia kile kinachoelezwa kuwa ' ombi lake mwenyewe'. 
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kitaifa huko Saudi Arabia.
Taarifa kwamba Prince Bandar bin Sultan anaondoka kama mkuu wa shirika la kijasusi la Saudi Arabia zilipokelewa kwa shangwe na mahasimu zake, ikiwa ni pamoja na Iran na washirika wake wakuu, Syria na kundi la Hezbollah la Lebanon.

Televisheni ya Iran Al Alam inamlaumu Prince Bandar kwa kuunga mkono al- Qaida huko Syria  ikisema  kuanguka kwake kisiasa  kunatokana na kushindwa kwake kumwangusha  rais wa Syria Bashar Al Assad.

Nafasi ya Prince Bandar mwenye umri wa miaka 65, inachukuliwa na Jenerali Youssef Al Idrissi.

Bandar amekuwa akiongoza juhudi za Saudia za kumwondoa madarakani rais Assad wa Syria katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na kwa kuunga mkono baadhi ya makundi ya waasi wa dhehebu la Sunni nchini humo.

Pia anashtumiwa kwa kuunga mkono mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na hivyo kuchochea Mfalme Abdallah kumvua wadhifa wa kuongoza operesheni za Syria hapo mwezi Februari na kuukabidhi wadhifa huo kwa waziri wa masuala ya ndani Prince Mohammed Bin Nayef.

Profesa wa chuo cha American University mjini Beirut, Hilal Khashan, ameandika kuhusu Prince Bandar. Aliiambia Sauti ya Amerika kwamba kuunga mkono al-Qaida ni suala tete katika ufalme huo.

Prince Bandar ni mtu anayefahamika vyema mjini Washington ambapo aliwahi kuwa balozi wa Saudia  kwa Marekani kwa takriban miaka 30. 
 
Pia ana uhusiano mzuri na marais wa zamani George W. Bush na babake George H. Bush.

0 comments:

Post a Comment