Dec 4, 2013

Kiongozi wa Kishia auawa

Kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Pakistan ameuawa na watu wenye silaha pamoja na mlinzi wake katika mji wa Karachi. 

Duru za usalama zimeripoti kuwa, Allama Deedar Ali Jalbani alifyatuliwa risasi na watu wenye silaha waliokuwa wamepanda pikipiki na baada ya kumuua walikimbia. 

Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mauaji hayo lakini kwa kawaida mauaji kama hayo hufanywa na makundi ya wanamgambo wa Taliban. 

Mashambulizi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Pakistan ambao idadi yao ni theluthi moja ya wananchi wa nchi hiyo yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, mamia ya Mashia waliuawa Pakistan mwaka 2012, huku jumuiya ya Mashia nchini humo ikiilalamikia serikali kwa kutochukua hatua madhubuti ili kuzuia mauaji hayo.

0 comments:

Post a Comment