Nov 9, 2013

Wakulima Wameyakimbia Mashamba Kwa Sababu Ya Njaa-WFP

Watu milioni moja wanakabiliwa na njaa CAR

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetahadharisha kuwa asilimia 20 ya jamii ya watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakabiliwa na baa la njaa na ukosefu wa chakula kutokana na mavuno dhaifu na machafuko yasiyokwisha.

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa raia zaidi ya milioni moja huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hawawezi kukidhi mahitaji yao ya chakula ya kila siku kama kawaida na kwamba huhitajia msaada wa chakula ili kudhamini mlo huo. 

Wakulima wengi wameyakimbia mashamba yao, na hivyo kuacha mazao bila ya uangalizi.  Imeongeza taarifa ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema linahofia kuwa usambazaji wa chakula kilichosalia katika msimu wa mavuno uliopita huwenda ukamalizika mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2014, miezi minne kabla ya muda wake wa kawaida. 

Ripoti ya hivi karibuni ya umoja wa Mataifa imewanyoshea kidole cha lawama waasi wa Seleka kwa machafuko mengi yanayojiri  huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

0 comments:

Post a Comment