MZEE NASSOR MOYO AMBAYE NI MWENYEKITI WA KAMATI YA MARIDHIANO ZAZNZIBAR.
Zanzibar. Kamati ya Maridhiano imetoa maoni yake ya Rasimu ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutaka Zanzibar ijitegemee karibu kwa kila
kitu.
Maeneo inayotaka yaondolewe kwenye Muungano ni uraia na uhamiaji, sarafu na
Benki Kuu, mambo ya nje na usajili wa vyama vya siasa.
Kamati hiyo inayounga mkono muundo wa muungano wa Serikali tatu inayoongozwa
na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo, iliwasilisha mapendekezo hayo juzi
katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusema kuwa maoni hayo ndiyo
mawazo ya Wazanzibari wengi.
Mapendekezo hayo yalisomwa na Mwakilishi wa Mji Mkongwe ambaye pia ni mjumbe
wa kamati hiyo, Ismail Jussa katika Kongamano la Katiba lililoandaliwa na
kamati hiyo.
Msimamo wa kamati hiyo unaelezwa kuwa chanzo cha mmoja wa wajumbe wake,
Mansour Yussuf Himid kuvuliwa uanachama wa CCM, Agosti 26 mwaka huu.
Akisoma mapendekezo hayo, Jussa alisema kwa kuwa Muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Zanzibar uliziunganisha nchi zilizokuwa huru, unatakiwa kuitwa
Muungano wa Jamhuri za Tanzania, kusisitiza kuwa rasimu hiyo inatakiwa kueleza
wazi kwamba nchi nyingine zinaweza kuingia kwenye muungano huo.
Alisema kamati hiyo imependekeza kuwa mambo ya nje yasiwe suala la muungano
na badala yake nchi washirika zisimamie zenyewe eneo hilo.
Alisema kwa kuwa muungano umetokana na nchi mbili zilizokubali kuungana na
kuunda shirikisho, msingi wa uraia wa shirikisho utokane na msingi wa mtu kuwa
raia wa nchi mshirika na si kinyume chake.
“Kila nchi mshirika (Zanzibar na Tanganyika), ibakie na uraia wake na mtu
kuwa na uraia wa nchi mshirika ndiko kumpe uhalali wa kuwa raia wa shirikisho,”
alisema.
Pia kamati imependekeza Rais wa muungano ambaye atakuwa na madaraka ya juu
katika shirikisho lote kwa mambo yote ya Muungano, hivyo nchi washirika
zinapaswa kuwa na haki sawa katika kutoa watu wa kushikilia Baraza la Mawaziri
la Muungano, Bunge na Mahakama.
Alisema rasimu inatakiwa itamke wazi kwamba urais wa Muungano utashikwa kwa
zamu na kwa kupokezana baina ya nchi washirika yaani Tanganyika na Zanzibar na
kwamba Rais atangazwe mshindi baada ya kupata kura zaidi ya asilimia 50 kutoka
Tanganyika na Zanzibar.
Mambo ya kuondolewa
Alisema uchumi si suala la Muungano hata katika Katiba ya sasa na kwamba nyenzo
za kuendeshea na kusimamia uchumi wa nchi kwa maana ya sera za fedha na uchumi
zimeendelea kudhibitiwa kupitia Serikali ya Muungano.
“Vyombo vikuu vinavyosimamia sera hizo ambavyo ni Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha ya Serikali ya
Muungano vimekuwa vikifanya uamuzi na kuyatekeleza bila ya kuzingatia kuwa
Zanzibar inategemea uchumi wa utoaji huduma na haiwezi kuwa sawa na uchumi wa
Tanganyika ambao unategemea rasilimali,” alisema.
Akizungumzia usajili wa vyama vya siasa alisema Rasimu ya Katiba haipaswi
kujumuisha suala la vyama vya siasa katika mambo ya Muungano na kwamba Zanzibar
na Tanganyika zinatakiwa kuandikisha vyama vyake vya siasa.
Alisema badala ya kuendeleza mfumo uliopo sasa wa Makamu wa Rais kupatikana
kutokana na mgombea mwenza, marais wa nchi washirika (Zanzibar na Tanganyika)
moja kwa moja wawe makamu wa kwanza na makamu wa pili wa Rais wa Muungano.
ISMAIL JUSA LADHU MJUMBE WA KAMATI YA MJI MKONNGWE ZANZIBAR.