MHE SHUKURU KAWAMBWA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO
ROBO tatu ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Uhuru iliyopo Manispaa ya
Shinyanga, wamezuiwa kufanya mitihani ya muhula wa pili kwa madai ya wazazi wao
kushindwa kulipia michango mbalimbali.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, waliozungumza na waandishi
wa habari mjini hapa juzi, walisema pamoja na kuzuiwa kufanya mitihani hiyo,
walimu wao waliwapa adhabu ya kukaa chini wakiwa juani na baadae walipewa kazi
ya kumwagilia bustani wakati wenzao wakiendelea na mitihani.
Mmoja wa wanafunzi hao (jina tunalo), alidai kuwa walielezwa na walimu wao
kwamba yeyote ambaye hatokuwa amelipa ada na michango mbalimbali shuleni hapo ikiwemo
mchango wa mlinzi hatoruhusiwa kufanya mitihani hiyo hadi watakapokuwa wamelipa
michango wanayodaiwa.
Mwanafunzi huyo alifafanua kuwa hata walipojaribu kuwaomba walimu wawaruhusu
kufanya mitihani kwa vile suala la michango si jukumu lao bali la wazazi,
walimu waligoma.
“Tuliwabembeleza sana
walimu waturuhusu kufanya mitihani hasa wale wa kidato cha nne na cha pili
kwamba matokeo ya mitihani hiyo kwa kawaida hujumuishwa na matokeo ya mwisho ya
kumaliza kidato cha nne lakini wakakataa.
“Binafsi niliwaeleza kuwa hivi sasa Serikali imetangaza mpango wa matokeo
makubwa sasa hivyo waturuhusu, lakini walimu hao walibeza na kueleza bila
michango kulipwa hakuna Big results now, tulishangaa, tukaambiwa wote ambao
hatujalipa michango na ada tukae chini uwanjani, hawakujali jua, kisha tukapewa
kazi ya kumwagilizia bustani,” alieleza mwanafunzi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule Msaidizi, Kasuka Masanja alikiri kuzuiwa kwa
watoto hao kufanya mitihani kutokana na wazazi wao kutokulipa michango waliyotakiwa
kulipa, lakini hata hivyo alidai mitihani hiyo si halisi bali ilikuwa ni
majaribio ili kuwashinikiza wazazi kulipa ada na michango wanayodaiwa.
Akizungumzia hali hiyo ofisa elimu sekondari Manispaa ya Shinyanga, Victor
Emmanuel, alishangazwa na taarifa za watoto hao kuzuiwa kufanya mitihani yao na kwamba ni kinyume
na maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
“Siamini kama kweli wanafunzi hao wamezuiwa kufanya mitihani yao, si
utaratibu, suala la michango haliwahusu watoto, ni la wazazi na tuliishatoa maelekezo
ya jinsi ya kufuatilia michango hiyo kwa wazazi kwa utaratibu wa kuwasiliana na
viongozi wa serikali katika kata, hairuhusiwi kabisa watoto kurudishwa nyumbani
kwa kutolipa ada ama michango,” alieleza Emmanuel.
Hata hivyo, Emmanuel aliahidi kulifuatilia tatizo hilo
ili kuweza kubaini ukweli wake ambapo alitoa mwito kwa shule nyingine kutozuia
wanafunzi kufanya mitihani yao
kwa sababu ya wazazi wao kushindwa kulipa ada ama michango au kuwapa adhabu ya
aina yoyote kwa makosa ambayo si ya kwao.