RAIS ALIYEONDOLEWA MADARAKANI MUHAMAD MORSI
Kiongozi wa mashtaka nchini Misri, amependekeza kuwa aliyekuwa
rais Mohammed Morsi afunguliwe mashtaka kwa kosa la kuchochea mauaji ya
waandamanaji.
Tuhuma hizo zinahusiana na ghasia zilizotokea nje ya ikulu ya rais mjini
Cairo Disemba mwaka jana ambapo angalau watu saba waliuawa kwenye makabiliano.
Aidha Wanachama wengine 14 wa vuguvugu la Muslim Brotherhood pia
wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka kuhusiana na makosa hayo hayo.
Bwana Morsi amekuwa akizuiliwa katika eneo lisilojulikana tangu kuondolewa
mamlakani mwezi Julai .
Anakabiliwa na mashtaka kadhaa ingawa pendekezo hii la yeye kushtakiwa ni la
kwanza tangu sokomoko kuanza Misri baada ya kuondolewa kwake mamlakani.
Tangu aondolewe mamlakani serikali ya sasa inayoungwa mkono na jeshi,
imekuwa ikiwasaka wanachama wa vuguvugu la Brotherhood wanaotaka bwana Morsi
arejeshwe mamlakani.
Mwezi jana mamia ya waandamanaji walifariki wakati vikosi vya usalama
vilipovamia kambi zilizokuwa zimekaliwa na wafuasi wa Morsi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mnamo siku ya Jumapili mwendesha mkuu wa
mashtaka alipendekeza kuwa Morsi afunguliwe mashtaka.
Walisema Morsi anashtakiwa kwa kuchochea mauaji na ghasia mnamo mwezi
Disemba mwaka 2012.
Hata hivyo haijulikani ni lini kesi hiyo inayohusiana na makabiliano
yaliyotokea nje ya Ikulu ya Rais Disemba mwaka 2012, itasikilizwa.
Maelfu ya waandamanaji walikuwa wakipiga kambi nje ya jengo hilo usiku wa kuamkia terehe 4 Disemba
wakilalamika kuwa rais Morsi amejipa mamlaka makubwa kupita kiasi na pia
wakipinga mpango wake wa kutaka kubadilisha katiba ya nchi.
Iliarifiwa kuwa Morsi aliwataka wafuasi wake kupitia kwa waziri anayesimamia
idara ya polisi kukomesha maandamano ya kutaka aachiliwe huru lakini wakakataa.
Inaarifiwa walinzi wa Morsi waliwataka wafuasi wao kuja kuvunja maandamano
hayo. Angalau watu saba waliuawa kwenye makabiliano hayo.
Wafuasi wa Morsi wanasema kuwa walikuwa wanalinda eneo hilo baada ya kushambuliwa na wafuasi wa
upinzani.