Sep 2, 2013

TUNATAKA SERIKALI TATU-CUF



CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeendelea kusisitiza kuwepo kwa Muungano wa Serikali tatu na kueleza kuwa suala hilo ni muhimu katika kipindi hiki ili kurahisisha utendaji kazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Tanzania Bara.
Hayo yalibainishwa na Katibu wa Jumuia ya Wanawake wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Nuru Bafadhiri Awadh, wakati wa hafla ya ufunguzi wa tawi jipya la chama hicho la New Mauzi lililofunguliwa Kata ya Duga mkoani hapa juzi.

“Serikali tatu zinahitajika katika kipindi hiki, kwani zitaharakisha utendaji kazi kwa pande zote mbili badala ya Serikali mbili zilizopo sasa, ambapo kumekuwa ni mzigo kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya kazi hadi za Zanzibar ambazo kimsingi zingemalizwa na Wazanzibar wenyewe,” alisema Awadh.

Pia alisema kuwa chama hicho ndicho kilikuwa cha kwanza kupendekeza kuwepo kwa Serikali tatu na kudai Katiba mpya ili kuwepo kwa uhalisia wa utanganyika.

Alisema wakati huu ni wakati wa kushikamana kwa vyama vyote na dini zote badala ya kuanza kubaguana jambo ambalo ni hatari kwa taifa.

Wakati huohuo, Diwani wa Kata ya Mwanzange, Rashid Jumbe alisema suala la wananchi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji linatokana na huduma duni zinazotolewa katika zahanati na hospitali za umma.

“Tusimtafute mchawi, ongezeko la wananchi kwenda kupata matibabu kwa waganga wa jadi linachangiwa na huduma mbovu zinazotolewa na hospitali za serikali,” alisema Jumbe.

Akizungumzia kukithiri kwa uingizaji wa dawa za kulevya, alisema suala hilo linachangiwa na watendaji wa Serikali wasio waaminifu kwa kushirikiana na wafanyabiashara.

Katika uzinduzi huo, chama hicho kilipata wanachama wapya 73, ambapo walikabidhiwa kadi papo hapo na kujigamba kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chama hicho kitaongoza Halmshauri ya Jiji la Tanga.