Sep 4, 2013

WABUNGE ZANZIBAR NGANGARI,WAUKATAA MUSWADA

  • Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano.
Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa utajadiliwa Bunge lijalo.

Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema kwamba kuahirishwa huko kumetokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.

Muswada huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika kikao cha Bunge kinachoendelea ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.

“Ukisoma huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa Tanzania Bara na Zanzibar sasa sheria hii ina apply vipi (inatumikaje) Zanzibar wakati kule tuna sheria yetu tayari?” alihoji Mbunge mmoja wa Zanzibar.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana, alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na utakaojadiliwa ni ule wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.

“Bunge litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni kweli huo Muswada wa Kura ya Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko kwenye ngazi ya kamati,” alisema Joel.

Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa muswada ambao ulishaingizwa kwenye ratiba ya Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.
“Ni kweli muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili bado kuna mashauriano yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo waliokwamisha muswada huo kutokana na mgongano wa sheria.

“Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano,” alisema.

Lissu alisema tangu mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha Kamati ya Bunge kwamba mapendekezo hayo yana upungufu.