Mahakama ya kijeshi nchini Misri imetoa hukumu ya vifungo vya
muda mrefu jela kwa wafuasi wa Rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi.
Watu hao walihukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia wanajeshi.
Mmoja wa washukiwa alifungwa jela maisha, wengine watatu wakipewa vifungo
vya kati ya miaka 5, 15 na 45, kwa mujibu wa taarifa za jeshi.
Walishtakiwa kwa kuwafyatulia risasi wanajeshi wakati wa ghasia na vurugu
katika mji wa bandarini wa Suez
mwezi jana.
Vurugu hizo zilitokea baada ya msako mkali uliofanywa na maafisa wa usalama
dhidi ya wafuasi wa Moris waliokuwa wamepiga kambi mjini Cairo.
Mamia ya watu, wengi wao wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood,
waliuawa wakati wafuasi wa Morsi walipokuwa wamepiga kambi nje ya msikiti wa
Rabaa al-Adawiya na katika medani ya Nahda wakitaka Morsi aachiliwe, ingawa
waliondolewa kwenye kambi hizo tarehe 14 mwezi Agosti.
Vurugu zilizotokea mjini Suez, Mashariki mwa Cairo, kati ya tarehe 14
na 16 mwezi Agosti zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 30.
Hata hivyo haijulikani ikiwa wale waliohukumiwa Jumanne ni wanachama wa
Brotherhood. Lakini ikiwa ni wanachama wa vuguvugu hilo,
hukumu walizopewa bila shaka zitaathiri sana
chama hicho hasa ikizingatiwa ni za kwanza kutolewa kwa vugu vugu hilo tangu kuondolewa
mamlakani kwa Morsi.
Viongozi wa mashtaka walitangaza tarehe 1 Septemba miezi miwili baada ya
kuzuiliwa kwa Morsi kuwa anatufunguliwa mashtaka kwa kuchochea mauaji.