Kiongozi mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu,Sheikh Khalid
Azzan Hamdan amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja akiwa chini ya ulinzi wa
askari Magereza na polisi kuanzia Septemba Mosi mjini hapa imefahamika.
Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar
(Magereza), Khalifa Hassan alisema Azzan aliwahi kuishiwa nguvu za miguu mara
mbili akiwa katika mahabusu ya Gereza la Kinuai,Mkoa wa Mjini Magharibi
kisiwani Unguja.
Hassan alisema,kufuatia hali hiyo, magereza waliamua kumpelekea katika
hospitali hiyo ya Mnazi Mmoja na kuamriwa alazwe kwa uchunguzi zaidi na
matibabu kufuatia afya yake kuzorota ghafla. Alisema, watuhumiwa wengine
wanaokabiliwa na kesi ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa
Taifa mbali na Azzan, wanaendelea vizuri na wako katika afya njema ambapo jana
walifikishwa mahakamani bila ya mshtakiwa mwenzao huyo kuwapo.
Wakili wa washtakiwa hao, Abdallah Juma alisema baada ya kupokea taarifa za
mteja wake kuwa mgonjwa, aliamua kumjulia hali akiwa hospitali, lakini askari
walioimarisha ulinzi katika chumba cha wagonjwa wa mahabusu na wafungwa
walisema hawawezi kumruhusu bila ya kupewa kibali cha uongozi wa magereza Zanzibar.
Hata hivyo, Wakili Abdallah alisema, mteja wake Azzan anasumbuliwa na
matatizo katika kibofu cha mkojo kutokana na kuwa na vijiwe ambapo alitakiwa
kutibiwa nchini India
na Afrika Kusini.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,Omar Abadllah Ali alisema kwamba tayari
daktari anayemshughulikia ameshachukua vipimo muhimu na anaendelea kufanya
vipimo maalumu kwa kutumia mashine ya picha.
Hata hivyo alisema ni mapema kuyazungumzia maradhi yanayomsumbua mtuhumiwa
huyo, lakini alikiri na kusema amelezwa katika chumba maalumu hospitalini hapo.
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wana familia za viongozi wa Uhamsho kwamba
wamekuwa hawapewi fursa stahiki kuonana na ndugu zao walioko mahabusu sambamba
na kuteswa na kunyanyaswa kwa viongozi hao ambao hadi sasa wamenyimwa dhamana
kwa muda mrefu.