MANSUOR YUSUPH HIMID AKIONGEA KATIKA UKUMBI WA BWAWANI ZANZIBAR
- Huku akizungumza kwa umakini na kujiamini alisema, “ "CCM kimejaa ubaguzi, siasa za chuki na kimeshindwa kusimamia misingi imara ya kutetea masilahi ya wananchi. Wazanzibari kataeni hali hii, wekeni tofauti za vyama pembeni, Zanzibar kwanza vyama baadaye. Tusimamie muungano wa heshima, haki na usawa".
Siku saba tangu Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (Nec), kumvua uanachama,
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf
Himid, kutokana na kukiuka miiko ya chama hicho, ameibuka jana na kukiponda
chama hicho kuwa kimejaa siasa za chuki na ubaguzi.
Huku akizungumza kwa umakini na kujiamini alisema, “ CCM kimejaa ubaguzi,
siasa za chuki na kimeshindwa kusimamia misingi imara ya kutetea masilahi ya
wananchi. Wazanzibari kataeni hali hii, wekeni tofauti za vyama pembeni, Zanzibar kwanza vyama
baadaye. Tusimamie muungano wa heshima, haki na usawa.”
Himid ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar yenye wajumbe sita,
alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la wazi lililoandaliwa na kamati hiyo
katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani na kuongozwa na mwanasiasa mkongwe ambaye
pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo.
Katika hotuba yake ya dakika 46, Mansour ambaye kwa nyakati tofauti amewahi
kuwa Waziri na Naibu Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Waziri wa
Kilimo, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la
Zanzibar, aliendelea kusimamia msimamo wa muundo wa muungano wa serikali tatu
kwa kufafanua kuwa, “Muundo wa muungano wa serikali tatu ni wimbi kubwa
halizuiliki tena.”
Mansour ambaye alisema hajui sababu za kufukuzwa kwake CCM, alisisitiza:
“Sitakwenda mahakamani kukata rufaa kwa sababu nilichaguliwa na wananchi hivyo
sitaki kuwawakilisha kwa mgongo wa mahakama,”
“Pia sina pesa za kuchezea huko mahakamani. Sihitaji malumbano, katika
uchaguzi mdogo sitagombea kwa sababu sitaki kuendeleza machungu kwa wananchi wa
jimbo langu na pia najiepusha na siasa za matusi, naweza kufikiria kugombea
mwaka 2015.”
Akigusia suala la Muungano Mansour amesema ataendelea na harakati zake kusimamia maslahi ya Zanzibar ili
kuona mchakato wa Katiba Mpya unakuja na Katiba yenye Muundo wa Muungano wa
Haki na Usawa baina ya Tanganyika
na Zanzibar.
Katika kongamano hilo
mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mohamed Ahmed Al-riyami alitangaza kujivua
uanachama wa CCM, kwa maelezo kuwa chama hicho kimepoteza mwelekeo.