"IGP SAID MWEMA,MUASISI WA ULINZI SHIRIKISHI KWA NIA NJEMA,LAKINI WACHACHE WANAITUMIA VIBAYA FURSA HIYO."
Hali ya usalama kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (UBT), imekuwa
tete baada ya kuibuka kwa kundi kubwa la matapeli wanaowaibia abiria na
kuwabambikizia kesi kwa kutumia njia ya ulinzi shirikishi.
Mbali na kufanyika kwa vitendo hivyo kituo hicho kinadaiwa kuwa soko kubwa
la biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya Bangi na Mirungi.
Kundi hilo ambalo linajulikana kama vishoka limekuwa likifanya vitendo hivyo kuanzia saa
mbili usiku kwa kujifanya kuwa wao ulinzi shirikishi, na kufanya utapeli huo
kwa kuwakamata abiria na baadhi ya watu wanaoingia kwenye kituo hicho na kuwapa
makosa mbalimbali.
Aidha uchunguzi huo pia umebaini kwamba mchezo huo mchafu umekuwa ukifanyika
kwa muda mrefu ambapo tayari kundi kubwa la watu wametapeliwa na kuibiwa vitu
mbalimbali.
Uchunguzi huo umebaini kwamba moja ya utapeli unaofanywa na kundi hilo la vijana wanaojiita
ulinzi shirikishi, ni kutumia pete feki za dhahabu ambazo wanazitumia
kuwatapeli fedha abiria.
Pia, licha ya kufanya utapeli huo kwa kutumia dhahabu feki, kundi hilo linatumia bidhaa ya
sabuni kuwatapeli simu abiria. Sabuni hutengenezwa kwa mfano wa simu na
kuwabambika watu kuwa ni simu halisi.
Licha ya kufanyika kwa vitendo hivyo, uchunguzi pia umebaini kuwepo kwa
biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Uchunguzi pia umebaini kwamba vijana hao matapeli wakimkamata mtu kwa
kisingizio cha kuhusika na wizi, wanamtoza faini kati ya Sh50,000 hadi 70,000.
Makosa yanayodaiwa kuwa madogo kama kukojoa au
kutupa uchafu wanatoza faini ya kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 kila siku.
Akizungumzia suala hilo
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo (NHC), Amani Sizia alithibitisha
kuwepo kwa vitendo hivyo vya uhalifu na kudai kwamba UBT imegeuka kuwa shamba
la bibi kwa wahalifu.
Sizia alisema: “Kwa kweli hali ya kituo cha mabasi ya Ubungo na maeneo
jirani imekuwa mbaya sana,
kuna vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo ni feki zaidi ya vitano. Vikundi
hivyo vimekuwa vikifanya kazi ya kuwatapeli abiria.”
Alisema kwa kuthibitisha zaidi nyakati za usiku kila kibaka anageuka kuwa
mlinzi shirikishi, na kufanya kazi ya utapeli ili kujipatia fedha.
“Nashukuru sana
ndugu yangu mwandishi kwa kunitafuta UBT kwa sasa haifai, kuna vitendo vingi
vya uhalifu ambavyo vinafanyika nyakati za usiku. Kila kibaka ikifika wakati
huo anageuka kuwa mlinzi shirikishi,” alisema Sizia.
Waathirika wengi wa utapeli huo ni akina mama ambao mara kwa mara wamejikuta wanaliona chungu jiji la Dar es salaam kutokana na madhila hayo ambayo inaaminika yanafumbiwa macho na mamlaka husika.