Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Profesa Karim Manji
(wa pili kushoto) akifurahia na wenzake baada ya kufanikiwa kwa operesheni ya
kuwatenganisha watoto walioungana, kazi iliyofanywa na jopo la madaktari bingwa
saba kwa masaa manne.
Jopo la Madaktari Bingwa Saba wa Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa ya hospitali hiyo (Moi),
wamefanikiwa kuwatenganisha pacha waliokuwa wameungana kiwiliwili.
Iliwalazimu mabingwa hao kutumia saa nne kufanikisha upasuaji huo. Mmoja wa
watoto hao waliotenganishwa, amelazwa kwenye Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU)
Taasisi ya Mifupa Moi wakati kiwiliwili kingine kilifariki.
Jopo la madaktari waliofanikisha upasuaji huo ni; bingwa mstaafu wa watoto
ambaye aliitwa maalumu kwa kazi hiyo, Petronila Ngiloi, Dk Robert Mhina
(mifupa) na Profesa Karim Manji aliyekuwa akifuatilia kwa karibu mapigo ya
moyo.
Wengine ni Dk Karima Khalid aliyekuwa akiratibu dawa ya usingizi, Dk Hamis
Shaaban (ubongo na uti wa mgongo), Dk Zaitun Bokhary (bingwa upasuaji watoto)
na Dk Nyangasa (moyo na mishipa ya fahamu).
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Dk Shaaban alisema walimfanyia vipimo
mtoto ambaye hakuwa amekamilika na kugundulika kuwa hakuwa amekamilika viungo
vyote achilia mbali kutokuwa na kichwa na macho pia hakuwa na moyo, figo,
tumbo, maini ila alikuwa na uti wa mgongo.
“Uti wa mgongo ulikuwepo na ndio uliokuwa umeshikana na mwenzake na kuna
mshipa mmoja wa fahamu ulikuwa unafanya kazi ndio maana alikuwa ukimgusa
anachezesha mguu.”
Alisema kinachoratibiwa kwa sasa ni kuangalia dawa ya usingizi aliyopewa
mtoto ambaye anaendelea kupumua na kwamba ndani ya saa 24, dawa ya usingizi
waliyomuwekea mtoto huyo itakuwa imeisha na ataanza kunyonya kama
kawaida.
Kazi ya upasuaji huo ilianza saa mbili asubuhi kwa mtoto huyo wa jinsi ya
kike aliyetimia kuchukuliwa vipimo mbalimbali ikiwemo CT Scan, MRI, Ultra sound
na vingine vingi kabla ya upasuaji kamili kuanza saa tano asubuhi.
Dk Shaaban alisema ni mara ya kwanza kwa Moi kufanya upasuaji wa aina ile na
kwamba mara nyingi wamekuwa wakifanya upasuaji wa watoto wanaozaliwa na vichwa
vikubwa pamoja na mgongo wazi ambao tatizo hilo linasababishwa na upungufu wa
madini ya folic acid.
Kabla ya upasuaji kuanza, mama wa mtoto huyo Pili Hija (24) alitumia muda wa
nusu saa kufanya maombi maalumu ya kumwombea mtoto wake kisha kuwaruhusu
madaktari kuendelea na upasuaji huo.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuruhusiwa kumwona mtoto wake, Hija alisema:
“Ninamshukuru Mungu kwa yote na nazidi kumwomba amjalie mwanangu apone kabisa,
nawashukuru na nitazidi kuwaombea madaktari wanaomtibu mwanangu.”