Mar 21, 2016

Hofu ya Ebola yatanda Tanzania, wawili wafariki Dar


Hofu ya Ebola yatanda Tanzania, wawili wafariki Dar
Hofu ya Ebola imetanda nchini Tanzania baada ya watu wawili kufariki dunia jijini Dar es Salaam wakiwa na dalili za homa hiyo hatari.

Watu hao walifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam wakiwa wanatoka damu sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo kwenye ngozi, mdomoni, puani na matundu mengine ya mwili.

Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa katika hospitali ya Muhimbili, Dk Praxeda Ogweyo amesema kuwa, wamewapokea wagonjwa hao wawili, lakini vipimo havijaonyesha kama wana ebola. 

Taarifa za awali zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu zinaeleza kuwa wagonjwa hao wote walipita Mafinga, Iringa kabla ya kuja Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kwamba, wizara yake imepokea taarifa hizo: Amesema kama ninavyomnukuu: 

“Tumepeleka sampuli kwenye Maabara ya Taifa, majibu yote yanaonesha kuwa, hawana ebola. Hata hivyo, tumeamua kupeleka nje ya nchi kwa ajili ya kujiridhisha zaidi."

Taarifa ya kuaga dunia watu hao wawili kwa dalili za homa ya Ebola ambayo ilipelekea watu wengi kufariki dunia katika nchi tatu za magharibi mwa Afrika za Liberia, Guinea na Sierra Leone imezua wasiwasi miongoni mwa raia hasa katika jiji la Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment