Feb 7, 2015

Waislamu watoa Tamko

Jumuia na Taasisi za Kiislamu   Tanzania
zimesema kuwa zitahamasisha Wanajumuia
wake kususia kupiga kura za maoni ya Katiba
mpya hadi pale watakapopata uhakika wa
kupata Mahakama ya Kadhi yenye meno.

Kauli ya Jumuia na Taasisi za Kiislamu zipatazo
11 imetolewa jana Jijini Dar es Salaam, na
kusomwa na Naibu Katibu wa Jumuia ya Shura
ya Maimamu Wilaya ya Kinondoni, kwa madai
kuwa kinachoendelea katika mchakato wa
kupatikana Mahakama hiyo ni hadaa za Serikali
zinazofanyika miaka yote hasa kinapofika
kipindi cha kupiga kura kwa lengo la kupata
kura za waumini hao.

Akizungumza kwa niaba ya baadhi ya Jumuia
11 za Kiislamu zilizosajiliwa na kutambulika
Kisheria ambazo ni Baraza Kuu, Tampro,
Basuta, Jasuta, IPC, Haiyat Ulamaa na Shura ya
Maimamu Tanzania, Shekhe Katiba alisema
kuwa watawahamasisha Waislamu wanaounda
Jumuia hizo kutopiga kura ya maoni wala
kushiriki kwa namna yoyote ile katika
mchakato wa kupatikana Katiba mpya kwa
sababu haiitambui Mahakama yao yenye haki
ya kuamua pindi kunapokuwa na tatizo upande
wao.

Alisema kuna baadhi ya Taasisi za kidini,
magazeti, kwenye mchakato wa kutoa maoni
juu ya Muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi,
umepotoshwa kwa kuituhumu Mahakama hiyo
kuwa italeta vurugu ikiwamo kuhukumu kwa
kukata watu mikono, kuhukumu wasiokuwa
Waislamu na kuwabagua wasiokuwa
Waislamu , Taasisi hizo 11 ni Wahabi hivyo
maoni yao hayawakilishi waislamu wengi, kuwa
umepotoshwa makusudi ukiwa na lengo la
hadaa kwa Waislamu.

“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na
Serikali wasitilie maanani maoni yaliyotolewa
na Taasisi hizo 11, ambayo kama yatafanyiwa
kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa
Mahakama ya Kadhi inakidhi matakwa ya
Sheria za Kiislamu na wajibu wake kama
mamlaka ya kutoa na kutenda haki, ”alisema
Shekhe Katimba.

Nae Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jumuia
hizo Mzee Mwinyikai, alisema kuwa katika
Muswada unaoendelea kujadiliwa kwa madai
ya kupatikana Mahakama ya Kadhi Mufti
amepewa jukumu la kuteua makadhi na
kutengeneza kanuni za Uendeshaji wa
Mahakama ya Kadhi ili hali Mufti sio chombo
cha kisheria.

Alisema hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti
isipokuwa uwepo wake unategemea katiba ya
BAKWATA, hivyo Mahakama ya Kadhi uwepo
wake utategemea uwepo wa Katiba ya Bakwata
inayounda ofisi ya Mufti.

Kukiwa na mgogoro
wa kikatiba Bakwata athari yake itaikumba na
Mahakama ya Kadhi. Hakuna duniani mtu
ambaye ofisi yake haiundwi na sheria kisha
sheria ikampa mtu huyo madaraka ya kuunda
chombo chenye mamlaka ya kisheria kama
Mahakama.

“Serikali inalijua hili lakini imefanya makusudi
kwa kusukumwa na nia yake ya kutopenda
kuona Waislamu wanakuwa na Mahakama ya
Kadhi ya ukweli na yenye meno inayoweza
kuamua kwa haki migogoro na matatizo yake,
madai ya kwamba Bakwata ni baba na Taasisi
nyingine ni watoto hayana ukweli na ndiyo
maana hata Kamati ya Bunge haikutoa mwaliko
kwa Bakwata pekee , ”alisema Mwinyikai.

Katika taarifa ya Jumuia hizo iliyosainiwa na
Shekhe Abdallah Bawazir ambaye ni Makamu
Mwenyekiti wa Hay Atul-
Ulamaa, ilisema kuwa
muswada unaojadiliwa ili kupatikana
Mahakama ya Kadhi ni kiini macho kwa sababu
una baadhi ya mambo yatakayoleta mgogoro
kati ya waislamu na waislamu ikiwamo kutoa
hiyari kwa mtu kufungua shauri katika
Mahakama ya Kadhi au ya Serikali
jambo hili limekusudiwa
kuifanya Mahakama
ya Kadhi iwe butu na kutoa mwanya wa
kutokea mgongano baina ya Mahakama ya
Kadhi na mahakama za kawaida ikiwa kila
upande katika mgogoro utaamua kufungua
shauri katika mahakama tofauti.
Alifafanua Muswada huo unaitaka Mahakama
ya Kadhi ijiendeshe yenyewe
bila kupata fedha
kutoka Serikalini kitu ambacho
hakiwezekani ,jambo ambalo halijawahi
kutokea sehemu yeyote duniani chombo kama
mahakama kujiendesha chenyewe.
“Zipo mahakama za makundi ya watu maalumu
ambazo zinaendeshwa kwa pesa za serikali
ambazo ni kodi za Watanzania wote. Mfano ni
kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi, Biashara
kwa nini mahakama itakayotafsiri sheria za
Kiislamu iwe nongwa?, ”ilisema na kuhoji
taarifa hiyo.

Kwa upande wa Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shura ya Maimamu
Wilaya ya Kinondoni Chambo Ally alisema
kuwa , Serikali inatakiwa kupeleka muswada
Bungeni wa kujadili kuwapo Mahakama ya
Kadhi badala ya kurekebisha vifungu vya
Sheria kama wanavyojaribu kufanya sasa.
Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwa Baraza la
Waislamu Tanzania ‘BAKWATA’ Mufti Mkuu wa
Tanzania, Shehe Issa Shaaban Simba alisema
kuwa hana cha kubishana wala kuchangia
katika hilo kwa sababu Kamati ya kudumu ya
Bunge ya Katiba Sheria na Utawala iliziita
Taasisi zote za Kiislamu ikiwamo na hizo 11 na
kila moja ikatoa maoni yake ya nini kifanyike
ili kuboresha muswada wa Mahakama ya
Kadhi.

Alisema wao kama Bakwata waliungana na
Serikali na kukubaliana nini kitoke, kibaki,
kiboreshwe, hivyo na hizo taasisi nyingine ule
ndiyo ulikuwa wakati wao wa kukubali,
kukataa, kutoa mapendekezo, kujadili, kama
hawakufanya hivyo hakuna haja ya kupigizana
kelele au kubishana.
“Sioni haja ya kubishana, kila Taasisi ilitoa
maoni yake mbele ya Kamati, bado haijakutana
na kutoa maamuzi, haijapeleka chochote
kikajadiliwe Bungeni, nafikiri kuna haja ya
kusubiri kusikia watasema nini, ”alisema Mufti
Simba.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Ummy
Mwalimu, alisema kuwa hawezi kulizungumzia
hilo kwa sasa hadi itakapotolewa taarifa rasmi.
“Siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa, subiri
taarifa rasmi kuhusiana na Mahakama ya
Kadhi, usiwe na wasi itatolewa wakati wa
kufanya hivyo ukifika, ”alisema Mwalimu.

0 comments:

Post a Comment