Jan 27, 2015

SERIKALI YA WATOA KHOFU WAKRISTO JUU YA MAHAKAMA YA KADHI

Serikali imetangaza kukutana na viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo ili kuzungumza nao kuwaondoa wasiwasi kuhusu muswada unaokusudia kutunga sheria itakayoitambua Mahakama ya Kadhi nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari, katika viwanja vya Bunge, mjini hapa jana.

Alisema serikali inakusudia kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini wasiwasi uliopo kwa viongozi hao unatokana na kutouelewa vizuri muswada huo pamoja na mahakama yenyewe.

"Tutawafikia, tutaomba kuzungumza nao ili tuweze kubadilishana mawazo vizuri. Na bahati nzuri viongozi wa dini ni wasikivu sana kwa sababu ndiyo walinzi wetu wa kiroho. Tukiwaomba kwenda kuwaona hawawezi kukataa," alisema Masaju.

Alisema tayari madhehebu zote za kidini zimekwishamkaribisha aende kuzungumza nao kuhusiana na suala hilo.

"Na mimi nitaenda na wasaidizi wangu na baadhi ya viongozi serikalini na hata walioko nje ya taasisi za serikali kuwaambia jamani kitu chenyewe ni hiki na hiki na hiki. Baada ya uelewa, tutabaki wamoja. Tanzania tunatengeneza sheria siku zote hizi iwa maridhiano," alisema Masaju.

Alisema siyo Wakristo tu, bali hata Waislamu wenyewe pia kuna mambo mengine wamepeleka serikalini, ambayo ni makubwa zaidi yanayowapa Wakristo wasiwasi na kusema nao pia watawafikia pamoja na madhehebu mengine.

Alisema haoni sababu ya viongozi wa dini kutofikia mwafaka na kusisitiza kuwa anaamini kwamba, watakubali.

Aliwaomba waandishi wa habari kuepuka kuripoti habari, ambazo zinaweza kuwagawa Watanzania.

Alisema fedha za kuendesha mahakama hiyo zitaendele kugharimiwa na Waislamu wenyewe na kwamba, suala la kwenda kwenye mahakama hiyo ni la hiari.

Masaju alisema maandalizi ya muswada huo yameshirikisha Waislamu kwa kiwango kikubwa na kwamba, serikali imeshauriana nao na kwamba, mchakato huo ni wa siku nyingi, uliokuwapo tangu enzi za utawala wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

"Hii serikali hii nayo ilipokuja awamu hii nao wakaendelea mpaka tukafikia hatua pale," alisema Masaju.

Aliongeza: "Kwa hiyo, Waislamu wenyewe hawa tumewa-engage kwa siku nyingi sana kwenye hili suala kupitia Bakwata na taasisi zake. Na Bakwata ndiyo inayotambulika kisheria. Ipo kisheria ile Bakwata. Lakini haina maana kwamba, walikuwa wanakuja Bakwata tu Waislamu wengine walikuwa hawaji, hapana."

Sasa baada ya kuelewana na Waislamu ndiyo unaona hata jinsi muswada ulivyo, wao wakaanzisha mahakama ya kadhi, sisi tunaona inahitaji inforcement kama haitambuliki.

Ndiyo maana unaona kwenda kule liwe la hiari ya mtu na kwa Waislamu

Alisema ana uhakika mchakato huo unaolenga kujenga maridhiano, ukikamilika utatengeneza kitu, ambacho kitawafanya Watanzania wote kubaki wamoja.

Masaju alisema tatizo la uelewa kuhusu muswada huo anahisi linachangiwa na hatua kutochukuliwa mapema ili kuwaelimisha sheria inayokusudiwa kutungwa na lengo la serikali, kwani hakuna katiba inayovunjwa kwa kuletwa mabadiliko hayo.

Hata hivyo, alisema ana matumaini kuwa baada ya zoezi wanalolifanya la kushauriana na makundi yanayohusika, hatimaye watafikia mwafaka na sheria itakayotungwa itakuwa nzuri inayoridhiwa na pande zote mbili.

"Kwenye hili suala, ambalo linagusa imani za watu, kwenye hili tunachohitaji sisi umoja wa taifa hili ubaki palepale. Tuendele kuwa wamoja," alisema Masaju.

Aliongeza: "Tukishakuwa wamoja kama vile, kukawa na amani, ndipo tunapoweza kufanya mambo yetu vizuri yakaenda. Ndipo uchumi unaweza ukakua. Watu na imani zao za dini wataendelea kuabudu kwa haki wanavyoona, hakuna dini ya mtu itakayoingiliaya mwingine kwenye mambo haya."

Alisema muswada huo unawahusu Waislamu tu na kwamba, hauwahusu Wakristo.

"Siku moja Yesu aliulizwa na mwanasheria mmoja, unajua wanasheria hawa hawakuanza leo. Akamuuliza, hivi ni amri ipi iliyo kuu? Yesu akamwambia mpende Mungu wako kwa akili zako zotena kwa roho yako yote, hii ndiyo kuu na ya kwanza, ya pili yafanana na hiyo, mpende jirani yako kama nafsi yako. Hapo ndipo unapokuja kuona kwamba ni suala ambalo ni kwa sababu tu hatujalielewa vizuri," alisema

Aliongeza: "Jirani yetu kwenye hili kwa nyinyi mlio Wakristo ni Waislamu. Suala haya masheria yanayokusudiwa kuletwa hayataingilia masuala, ambayo kimsingi yanasimamiwa na serikali. Kwa maana ya mambo yale yanayosimamiwa na Jamhuri, mambo ya makosa ya jinai."

"Haya yanabaki kwenye kusimamiwa na serikali kama kawaida. Mtofautishe na yanayotokea katika nchi nyingine za Kiislamu."

Alisema muswada huo hautamki kwamba, Tanzania itakuwa dola ya Kiislamu na kusema itabaki kuwa ni serikali isiyokuwa na dini, lakini ambayo ina wananchi, ambao wana dini.

"Na sisi serikali ni wajibu wetu ni kuwawekea mazingira mazuri watu wanapoamini, wanatekeleza mambo yao kwa amani kabisa," alisema Masaju.

Aliongeza: "Wasiwasi ni kutokana hatujapata elimu ya kujua. Na sisi serikali lazima tuchukue hatua responcibility. Kwa hiyo, suala hili watu wanaogopa kulizungumza kwa sababu na wao pengine kutolielewa vizuri."

"Lakini hili ni suala, ambalo liko wazi, hata ukiangalia muswada ule pale. Yale pale mambo yenyewe ni ya hiari. Hata ndani ya Waislamu wenyewe ni hiari. Muhibu Said anaweza akaamua kwenda pale au akaenda kwenye mahakama nyingine."

Alisema tayari Waislamu siku nyingi walishaanzisha utaratibu wa kuwa na Mahakama ya Kadhi na kwa hiyo, muswada huo unakusudia kutambua tu maamuzi yanayofanywa mahakama hiyo.

"Ombi langu mimi ni kwamba, mimi nilikuwa naomba tu nikuhakikishieni ndgu zangu, hapa serikali ndiyo wajibu mkubwa sana wa kuwaunganisha wananchi. Na serikali haiwezi kuleta kitu, ambacho kwa asili yake kinawagawa wananchi," alisema Masaju.

Aliongeza: "Nyinyi muiunge mkono serikali kwamba, muswada huu unaletwa kwa nia njema kabisa, hauwezi kuwa ndiyo chanzo sijui cha nini. Yaani, Kama ni kitu, ambacho unaishi na jirani yako, ambao nyinyi Wakristo mnapaswa mpende jirani yako kama nafsi yako."

"Mfano mzuri tu ni huu, mimi kwa sababu nilikuwa sijapata mifugo ya ng'ombe. Ardhi yangu nililima nikapanda na mazao, lakini wewe uliyekuwa na mifugo ambaye ni jirani yangu, ulipotengeneza uliacha na njia ya kupitisha mifugo. Baadaye, mimi ambaye sikuwa na mifugo, lakini eneo langu lile nililima lote, sikuacha njia ambayo ningepitisha mifugo. Sasa nakuja napata mifugo, nakwambia wewe jirani yangu ee bwana nimepata mifugo, nimeozesha binti yangu wewe unafahamu."

"Yule bwana kaniletea ng'ombe labda saba hivi, sasa naomba niwe napitishia mifugo yangu hapa kwenye njia yako hii ili nifikie nyumbani kwangu, ukikataa naye atakushangaa, huyu huyu unatakiwa umpende kama nafsi yako. Haiingii hiyo mifugo kwenye shamba lake, ataweza kunung'unika tu. Na hiyo ndiyo inayoweza ikavunja mahusiano yenu kama majirani."

Aliwaomba viongozi wa dini, ambao alisema anawaheshimu sana, kutokuwa na wasiwasi dhidi ya muswada huo kwani hauna nia mbaya.

"Sisi serikalini tumeupika kwa undani sana. Kama kwa namna yoyote ile unavunja katiba, tumekuta hautavuja katiba," alisema Masaju.

Aliwaomba waandishi wa habari kuepuka kuripoti habari zinazohusu suala hilo kwa namna ya uchochezi.

Alisema mbali na kukutana na viongozi wa dini, atakutana pia na wanahabari, hivyo akawaomba kila mwanahabari aandae na kisha ampelekee hoja zinazoonyesha namna kuwapo kwa mahakama hiyo kutavunja katiba ya nchi, kama baadhi ya watu walivyo na wasiwasi.

Hata hivyo, alisema haamini kama wabunge wanaweza kuwapo bungeni kwa ajili ya kuwasaliti wananchi.

Pia alisema kamwe hawezi kupeleka bungeni kitu ambacho kiko kinyume cha maslahi ya wananchi, kwani anaamini kufanya hivyo kunaweza kumpotezea sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

0 comments:

Post a Comment