Nov 23, 2014

Waislamu wa Kenya walalamikia kufungwa misikiti

Waislamu nchini Kenya wamelalamikia hatua ya polisi ya nchi hiyo ya kufunga misikiti kadhaa katika Kaunti ya Mombasa.
Waislamu wa nchi hiyo wamevitaka vyombo vya usalama vya Kenya kufungua misikiti ya Mussa, Swafa, Mina na Sakina ambayo ilifungwa hivi karibuni na polisi kwa sababu za kiusalama. 

Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wanaikosoa vikali hatua hiyo ya polisi ya Kenya ya kufunga misikiti hiyo wakisema hilo sio suluhisho la kupambana na ugaidi. 

Juma lililopita polisi ya Kenya ilivamia misikiti kadhaa katika Kaunti ya Mombasa na kuwatia mbaroni mamia ya vijana wa Kiislamu ikiwatuhumu kwa ugaidi. 

Polisi ya Kenya imetangaza kuwa, ilipata silaha katika misikiti hiyo, madai ambayo yanatiliwa shaka na baadhi ya Waislamu wa nchi hiyo. 

Aidha viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wanapinga vikali hatua ya polisi ya kufunga misikiti hiyo na kusisitiza kwamba, Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamwa katika vita dhidi ya ugaidi.

 Katika upande mwingine Wabunge wa Kenya katika mji mkuu Nairobi wameeleza masikitiko yao kutokana na kutokuwa na matunda hatua za kuimarisha usalama na kutahadharisha kwamba, kufungwa misikiti minne ya Mussa, Sakina, Swafa na Mina huko Mombasa ni kinyume cha kisheria na wametaka kuhitimishwa suala hilo.

0 comments:

Post a Comment