Sep 30, 2014

FUNDI SELEMALA AJINYONGA

KATIKA hali ya kushangaza, mtu mmoja ambaye ni fundi seremala aitwaye Emmanuel Carlos, mkazi wa Kwabinyau Magomeni jijini Dar amekutwa akiwa amejinyonga saa mbili asubuhi Septemba 23, mwaka huu katika kile kinachodaiwa kuchoshwa na mgogoro wa kifamilia.

Emmanuel Carlos enzi za uhai wake.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kwamba, kwa muda mrefu, marehemu alikuwa na mgogoro usioisha na mkewe Mariamu Suleimani uliosababisha wawili hao kulala katika vyumba tofauti ndani ya nyumba yao.

Baadhi ya majirani wa eneo hilo walisema kutokana na ugomvi huo, marehemu alikuwa akirudi nyumbani usiku akiwa amelewa na kumtukana matusi mkewe huku baadhi wakienda mbali na kudai alikuwa haachi hela ya matumizi.


Hata hivyo, mkewe marehemu anadaiwa kuwa na biashara yake ya samaki na alikuwa akijituma ili kuhakikisha anapata nauli ili arejee nyumbani kwao.

Mke wa marehehu akilia kwa uzuni.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana, mtu wa kwanza kujua kuhusu suala hilo alikuwa ni kijana wake mwenye umri wa miaka saba, Celestine Carlos aliyekwenda chumbani kwa baba yake kuomba hela ya shule, ambapo alimkuta akining’inia kwenye dari baada ya kuwa amejifunga kamba kwenye feni.

Akizungumza na waandishi wetu Mariamu alisema kuwa siku moja kabla ya tukio, mumewe alirudi nyumbani na kumtukana huku akilia na kumwambia kuwa atamkumbuka sana katika maisha yake na kwamba kabla ya kupambazuka mmoja wao atakuwa amekufa.


“Siku iliyofuata alipoamka alinikuta naosha vyombo, akanitazama kwa jicho baya kisha akaenda chumbani kwake ambako alijifungia.

Baadhi ya wananchi wakiwa eneo la tukio.
Nusu saa baadaye alikuja mwanaye Celestine na kuniomba hela ya shule, nikamwambia aende akachukue kwa baba yake, alipoingia akarudi na kuniambia baba yake ananing’inia, jambo nililoona kama utani lakini baadaye nilienda na kumkuta akiwa amejinyonga,” alisema Mariamu huku akilia kwa uchungu.

Naye mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Jumanne Mneka alikiri kufahamu mgogoro wa familia hiyo na kusema walikuwa wakiwasuluhisha kila mara.

Polisi wakiwa eneo la tukio.
“Juzi kati tu tumetoka kuwapatanisha, nashangaa leo saa mbili asubuhi napokea taarifa kuwa Emmanuel amejinyonga, nimehuzunika sana,” alisema.
Majirani wakiwa wameshtushwa na kushangazwa na jambo hilo, waliungana na wapita njia kwenda kushuhudia tukio hilo, hali iliyoufanya mtaa huo usipitike kwa muda.



Waandishi wetu waliwashuhudia polisi wakifika eneo hilo na kuuchukua mwili na kuupeleka katika Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya uchunguzi. 


Marehemu ameacha mke na watoto wawili 

Habari hizi kwa hisani ya GP

0 comments:

Post a Comment