Aug 7, 2014

UKATILI: Inspekta wa Polisi mbaroni kwa tuhuma za kuua mwanaye

Jeshi la Polisi linamshikilia Inspekta wake, Celestine Makene (40) kwa madai ya kumpiga hadi kumsababishia kifo mtoto wa kaka yake, Alerd Makene (16).

Makene anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 24, mwaka huu katika makazi ya polisi, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam na anashikiliwa katika Kituo cha Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema marehemu Alerd alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mbagala Kuu.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kifo chake unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa endapo itathibitika kuwa alitenda kosa hilo.
“Tunamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye pia ni askari polisi katika Chuo cha Polisi Kurasini, tutahakikisha kuwa haki inatendeka bila kujali nafasi aliyonayo mtuhumiwa,” alisema kamanda huyo.
Imedaiwa kuwa Makene alimwadhibu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mzazi wa jirani akimlalamikia kwamba Alerd alimpiga mwanaye hivyo kumtaka amkanye juu ya tabia hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, jirani ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema watoto hao walikuwa wakicheza mpira lakini kwa bahati mbaya Alerd alimpiga rafiki yake huyo usoni kwa mpira na baada ya kupigwa kwa mpira, alikwenda kwao kumshtaki.
“Usiku huo baba yake alimfungia chumbani na kumpiga kwa fimbo, ngumi na mateke kiasi kilichomfanya mtoto huyo kupiga kelele sana,” alisema na kuongeza kwamba majirani walijaribu kwenda kumwamulia lakini hakusikiliza.
Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa alisafiri kikazi Nairobi lakini akadai kuwa kabla ya kuondoka, aliamuru mtoto huyo asifunguliwe mlango.
Alidai kuwa baada ya mtoto huyo kulalamika sana, mama yake mdogo alimfungulia mlango na kumkuta akiwa amevimba uso na akivuja damu nyingi.
Alisema waliamua kumpeleka Hospitali ya Temeke kwa matibabu na alifariki dunia usiku wa Ijumaa Agosti Mosi.
“Baba yake alirudi haraka kutoka Nairobi alipopigiwa simu kuwa Alerd ana hali mbaya na alifahamishwa baada ya muda mfupi kuwa amefariki,” alisema.

0 comments:

Post a Comment