Aug 30, 2014

KIKWETE KUKUTANA NA UKAWA


 
Wakati Rais Jakaya Kikwete akikutana na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato wa Katiba, Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), limesema amani ya nchi iko mikononi mwa kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Kwa maana hiyo viongozi wa vyama vya siasa hasa vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanatarajiwa kusafiri hadi Dodoma kumfuata Rais Kikwete ambaye leo anaingia katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani hapa, iliyoanza juzi katika Wilaya ya Kongwa.
Baadhi ya viongozi ambao wanatarajiwa kushiriki mkutano huo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia.
 Pia katika orodha hiyo wamo Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na mwakilishi wa vyama visivyo na wabunge ndani ya TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa. 

Ukiondoa Kinana, viongozi wengine ni wajumbe wa Bunge Maalumu.
 Habari zilizopatikana juzi na jana Dar es Salaam na Dodoma na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu zinasema mkutano huo umepangwa kufanyika leo jioni baada ya Rais Kikwete kuhitimisha ziara yake katika Wilaya ya Chamwino na unaweza kuendelea hadi usiku kutokana na jinsi ratiba ilivyokaa.
 “Mkutano utafanyika hapa Dodoma katika muda wa saa 48 kuanzia sasa na Rais hatakutana na Ukawa kama ambavyo imekuwa ikidaiwa, anakutana na viongozi wa vyama vya siasa,” 
 Mwanzoni mwa wiki hii, Cheyo aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa Rais Kikwete alikuwa amekubali kukutana na viongozi wa vyama vya siasa wiki hii ili kuzungumzia mustakabali wa Katiba. 

Hata hivyo, alipoulizwa jana siku ya mkutano pamoja na mahali utakapofanyika, Cheyo hakuwa tayari kuzungumza chochote.
 Mkutano huo wa Rais na viongozi hao umekuja wakati ambao kamati za Bunge Maalumu zimekamilisha uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, bila kuwapo kwa wenzao wanaokaribia 120 ambao walisusia mchakato huo tangu Aprili 16, kutokana na kile walichodai kuwa ni kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda.
 Mara kadhaa Ukawa wamesisitiza kwamba kamwe hawatarejea bungeni hadi pale masharti yao yatakapotekelezwa na CCM kikishikilia msimamo wake kwamba masuala yote yanayohusu Katiba Mpya lazima yatatuliwe ndani ya Bunge. 

Kwa kuzingatia mazingira hayo ni dhahiri kwamba matokeo ya kikao hicho yanasubiriwa kwa shauku kubwa kwani yanaweza kusaidia kukwamua mchakato wa Katiba ambao umekosa uhalali wa kisiasa kutokana na Ukawa kuususia.
Mzigo wa amani
Wakati hayo yakiendelea Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) limetoa tamko kali kuhusu mchakato wa Katiba, na likiweka bayana kwamba ni Rais Kikwete pekee ambaye anaweza kukwamua suala hilo.
 Jukwaa hilo linajumuisha taasisi kubwa za madhehebu ya Kikristo ambazo ni Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA.)

0 comments:

Post a Comment