Mambo yamebadilika. Ukimya ulitawala jana katika Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, baada ya wabunge zaidi ya 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge hilo.
Ilikuwa ni saa 10:31 jioni baada ya Mjumbe wa
Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alipohitimisha uchangiaji wake akisema: “Ukawa hatuwezi kuendelea
kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni
kinyume cha matakwa yao.”
Baada ya kauli hiyo aliondoka akifuatiwa na
Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wao kutoka nje ya
Bunge.
Ukimya ulitawala takriban dakika mbili hivi na
baada ya wajumbe hao kutoka, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samia
Suluhu Hassan aliwaelekeza makatibu kuhesabu wajumbe ili kuona kama
akidi imetimia ili waendelee na kikao.
Baadaye aliliambia Bunge kuwa makatibu wamemweleza
hawahitaji akidi kwa kuwa kikao kilikuwa kinaendelea wakati Ukawa
walipotoka nje ya ukumbi.
Hotuba ya Lipumba
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu Gazeti la
Mwananchi la Aprili 14, mwaka huu katika sehemu inayosema; “Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) ameanza kampeni
kanisani kwa kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa
kuwa serikali ya muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.”
Alisema yeye ni muumini wa dini ya Mwenyezi Mungu
lakini anaafiki mapendekezo yaliyoletwa bungeni hapo na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais.
“Hii ni kauli ya Waziri Lukuvi ndani ya Kanisa la
Methodist wakati wa sherehe ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa
Askofu na Waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu.”
Alisema inasikitisha kwa sababu kauli hiyo inafanana na ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia Bunge Maalumu.
Alisema kauli za Lukuvi zinatisha baada ya kusema
Wazanzibari ambao wanataka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali
wanataka wapate nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu.
“Waziri anaweza kusema hivyo ndani ya kanisa?
Kawahamasisha mpaka yule kiongozi wa kanisa akasema ili kudumisha
Muungano bora Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja
ambayo inadumisha Muungano,” alisema.
0 comments:
Post a Comment