
Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Michael Jamson.
RAIS Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa mchakato mzima wa Katiba
baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka muundo wa Serikali mbili
badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika
ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua
hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi
18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa
na maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba, Rais Kikwete alisema suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda
mama katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio
sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku
akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo, Kikwete alisema kuwa wanaotaka
Serikali tatu waangalie changamoto zake na kuzitafutia majibu, kwa
maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika kirahisi.
Alisema
ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi kuwa Serikali tatu hazitakuwa
na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo huo una gharama na
utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM inaweza kuzimaliza kero
za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya tatu.
Huku
akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba sambamba na kuwapiga
vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo Christopher Mtikila (DP)
na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali
tatu;
“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo matakwa
ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar. Sababu ya pili muundo huo unatoa
majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa
Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”
Aliongeza,
“Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba muundo wa Serikali tatu ni
matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo wa Kiswahili wengi wape.
Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume kwamba hazionyeshi ukweli
huo.
Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu
siyo yangu.” Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu
wanasema Watanzania waliotoa maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820
sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu
303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano
na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”
Alisema
hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia 13.6 ndiyo wageuke Watanzania
walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka Serikali tatu.
“Watu
wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu takwimu (ukurasa 66,67),
inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu muungano watu
17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa na asilimia 37.2 na
waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8, Serikali ya mkataba
asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7” alisema. Alisema taarifa
ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa maoni ni asilimia 10.4
ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6
hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
“Watu wanahoji
kama Muungano ni jambo linalowakera sana Watanzania ingethibitika
kwenye wingi wa wale waliotoa hoja. Usahihi wa hoja hii ni upi,
nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia
sababu ya pili ya tume kwamba muundo wa Serikali tatu unajibu
changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku akifafanua kero
zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi ndiyo waamuzi,
sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume yenyewe imekiri
kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto zake ikiwa ni
pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma.
Mar 22, 2014
MUDA WA KUWA NA SERIKALI TATU BADO;RAIS KIKWETE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







0 comments:
Post a Comment