Siku moja baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu
walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi
waamue.
Akizungumza jana asubuhi, Jaji
Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba
hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni
kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali,
wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la
Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo
lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada
ya kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa
1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni
inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba
hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais
angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.







0 comments:
Post a Comment