Kuna njama. Maneno haya mawili ndiyo yametumiwa na pande mbili zinazopingana ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, kuelezea hali iliyojitokeza jana wakati wa kikao cha Bunge hilo kuhusu mvutano wa mabadiliko ya kanuni.
Njama zinazoelezwa na pande hizo ni za kuvuruga
mchakato wa Katiba Mpya, zikirejea yaliyotokea jana jioni ikiwamo
zomeazomea hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Samuel Sitta kuliahirisha Bunge hadi leo jioni.
Baada ya kuahirisha Bunge hilo, Sitta alikutana na
waandishi wa habari na kusema kwamba kuna njama za baadhi ya wanasiasa
kutumia vurugu kuhujumu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, badala ya
kujenga hoja.
Bila kuwataja wanasiasa hao, Sitta alisema ikiwa hawataki kuendelea na mchakato huo, basi waondoke na kuwaacha wenye nia njema.
“Wanasiasa hawa wamedhamiria kuvuruga mchakato wa
Katiba, tuhuma ambazo tumetuhumiwa leo na Lissu (Tundu) ni uongo na
uzushi, mimi sihusiki na kupeleka marekebisho ya kanuni kwenye Kamati ya
Kanuni na Haki za Bunge,” alisema Sitta.
Sitta alikuwa anajibu mchango wa mjumbe wa Bunge,
Tundu Lissu alioutoa mapema kwenye kikao cha jioni, akipinga
kilichoelezwa ni njama za kutaka kubadili kanuni kinyemela ili kumsaidia
mwenyekiti kulidhibiti Bunge.
Sitta alisema kwa kuzingatia kanuni ya 59 (1),
Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kupeleka marekebisho ya kanuni ili
kuliwezesha Bunge kufanya kazi vizuri.
Alisema hoja kwamba haiwezekani kufanyika
mabadiliko hata kabla ya kuanza kutumika kanuni, siyo ya msingi kwani
kila kitu kinabadilika kutokana na mazingira yake.
“Kamati ya Uongozi ndiyo ilipeleka waraka wa
mabadiliko ya kanuni kwa Kamati ya Kanuni na Haki kwa kuzingatia kanuni,
lakini hata kabla ya kujadiliwa na kamati husika inaonekana kuna
wajumbe ndiyo wameichukua na kuifikisha bungeni,” alisema Sitta.
Alisema kwa kiasi kikubwa marekebisho ambayo
yangesomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, yalilenga
kutoa ufumbuzi wa kanuni ya 37 na 38 juu ya upigaji kura ama uwe wa wazi
au siri.
Sitta alisema pamoja na hilo, kulikuwa na
marekebisho ya msingi kama kuweka utaratibu mzuri wa majadiliano katika
kamati pia kuweka utaratibu wa vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu hadi
Jumapili.
“Mengi ambayo alikuwa anayasema Lissu kama ni takataka hayakuwapo katika taarifa ya Kificho,” alisema Sitta.
0 comments:
Post a Comment