Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya Kikwete.
Amesema tayari amewaandikia barua Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa kuna njama za
kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; “Zanzibar ni
nchi” na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa
Wazanzibari kamwe hawatakubali kufanya hivyo.
Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka kwa Rais
Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa
Muungano kuwa wa serikali tatu.
Alisema Jaji Warioba aliweka kando itikadi yake ya
CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na
uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
“Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba
hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti
la Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza
Muungano wenye mfumo wa serikali tatu,” alisema Maalim Seif.
Alisema Muungano wa serikali mbili hauvumiliki na
kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza kutumia
sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka
jambo hilo.
“Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala
nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara
wanataka Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni
nchi, jambo hilo halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae,”
alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF.
Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba yake
alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala
yake akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.
Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na kutaja
ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi
litachukua madaraka ya nchi.
“Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu ni
wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga. Mambo
yamebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakuna atakayekusikiliza na
kubabaika,” alisisitiza Maalim Seif.
0 comments:
Post a Comment