Mar 29, 2014

Daesh yautangazia vita utawala wa Saudi Arabia

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daulatul-Islamiyyah fil-Iraq wa al-Sham kwa kifupi Daesh wametangaza vita dhidi ya Saudi Arabia. 

Wanamgambo hao sambamba na kuchana pasipoti zao na vitambulisho vyao vya uraia wa Saudia, wamemlaani pia mfalme Abdullah wa nchi hiyo.
Mwanamgambo mmoja wa kundi hilo amenukuliwa akisema kuwa, wanajitayarisha kurejea nchini Saudia kwa lengo la kuinua bendera ya jihadi na kusisitiza kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari kwamba, jihadi ndio mlango kuelekea peponi. 

Hayo yanakuja baada ya Saudia kuyatangaza makundi yote yanayoipinga serikali ya Riyadha yakiwemo ya Hizbullah ya Saudia, Jab'hatu Nusra na Daesh kuwa ni makundi ya kigaidi.

 Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh ambalo ni maarufu kwa kufanya jinai kubwa dhidi ya raia wasio na hatia nchini Syria na Iraq, wameenea katika mikoa ya Syria inayoshuhudia machafuko hasa mikoa wa AlRiqah, AlHasakah, Diruz-Zur, Aleppo na Idlib. 

Awali mfalme Abdullah wa Saudia alikuwa amewakataza wanamgambo kutoka Saudia wasiende tena Syria kupigana na jeshi la nchi hiyo, na kuyaweka makundi kadhaa katika orodha ya makundi ya kigaidi, hatua iliyotajwa na weledi wa mambo kuwa, na lengo la kuimarisha usalama ndani ya Saudia hasa kwa kukhofia kuwa, kurejea makundi hayo nchini humo kutahatarisha vibaya usalama wa nchi hiyo.

0 comments:

Post a Comment