Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Sakata la
wafanyabishara kuendelea kugomea mashine za elektroniki, limechukua sura
mpya baada ya maeneo mbalimbali kutangaza kuzikataa.
Juzi wafanyabiashara waliungana na kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati hasa kuhusiana na bei kubwa ya kifaa hicho.
Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)imewaonya
watu wanaowatisha wafanyabiashara hata kufunga maduka yao, kuwa kufanya
hivyo ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote
watakaokaidi.
Imebainisha taarifa hiyo kuwa TRA inasikitishwa na
kinachotokea hivi sasa kwani matumizi ya mashine hizo yalipitishwa
kisheria na Bunge la Tanzania mwaka 2011 na suala hilo lilitolewa
ufafanuzi na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal Novemba mwaka jana.
Wengine waliozungumzia sakata hilo ni, Rais Jakaya
Kikwete katika hotuba yake ya mwishoni mwa Machi 2011 pamoja na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
TRA imebainisha kuwa msimamo wa Serikali
unafahamika na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisisitiza kuwa suala
la matumizi ya mashine hizo ni la kisheria na wafanyabiashara hao
waliongezewa muda mara tatu wa kununua mashine hizo.
Wakati hayo yakiendelea, Chama cha Wafanyabiashara
wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA),kimeitaka Serikali kusitisha matumizi
ya mashine hizo na kuanza kushughulikia changamoto zilizotokana na mfumo
huo.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa
habari uliofanyika jijini jana, Rais wa chama hicho, Mhandisi Peter
Chisawillo alisema, Serikali inapaswa si kuwa sikivu pekee bali pia
kushughulikia kero zinazowakabili wafanyabiashara.
Dar es Salaam
Mgomo wa wafanyabiashara umeingia siku ya nne jana
na vikao baina ya Wizara, Mamlaka ya Mapato (TRA) na wadau wengine
vilikuwa vinaendelea bila kuwapo kwa dalili za mwafaka kupatikana.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa
Kodi, Diana Masalla, alisema utaratibu wa kutumia mashine utaendelea
hadi hapo, Wizara ya Biashara na TRA watakapotangaza vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment