Jan 24, 2014

Samba-Panza aapishwa kuwa Rais wa CAR

Meya wa zamani wa Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ameapishwa rasmi kuwa Rais wa muda wa nchi hiyo.

Bi. Catherine Samba-Panza ameapishwa baada ya kuteuliwa na Baraza la Mpito la nchi yake na anachukua nafasi ya Michel Djotodia aliyelazimika kujiuzulu majuma mawili yaliyopita baada ya kushadidi mapigano ya kikabila na kidini mjini Bangui na miji mingine ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Punde baada ya kula kiapo, Bi Samba-Panza ametoa wito kwa makundi ya Seleka na Anti-Balaka kuweka chini silaha na kufanya mazungumzo na serikali.

Huku hayo yakijiri, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa, Waislamu huko CAR wanakabiliwa na hali ngumu na kwamba wanaporwa pamoja na kuvamiwa na Wakristo walio wengi huku majeshi ya Ufaransa yakiangalia na hata wakati mwingine yamekuwa yakishangilia jinai kama hizo dhidi ya Waislamu.

Rais wa serikali ya mpito anatarajiwa kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki utakayoirudisha nchi hiyo kwenye mkondo wa demokrasia.

0 comments:

Post a Comment