MAPINDUZI
ya Zanzibar jana yalitimiza miaka 50, huku Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akielezea
mafanikio ya kupigiwa mfano, yaliyotokana na uongozi wa kizalendo katika
muda huo.
Kutokana na mafanikio hayo, Dk
Shein aliyehutubia Taifa jana kutoka Uwanja wa Amaan mjini hapa,
aliwataka Wazanzibari kuyaenzi Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, kwani
ndiyo yaliyowakomboa wananchi wa Unguja na Pemba na madhila ya wakoloni
ya utawala wa miaka 132.
Alisema Mapinduzi yalifungua utawala
wa kujenga heshima ya binadamu na kulinda utu na usawa wa kila mwananchi
bila ya kujali ubaguzi wa rangi. “Tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi
ya Zanzibar tukiwa huru katika nchi yetu na kufaidi matunda haya hatuna
budi kuwaombea dua waasisi wa Mapinduzi haya hayati Abeid Amani Karume
pamoja na wenzake,” alisema Dk Shein.
Aliwataka wananchi
kuimarisha umoja na mshikamano wa Mapinduzi na kukumbusha kuwa hata
kauli mbiu ya sherehe za Mapinduzi, imesisitiza umoja ndiyo nguvu ya
mwananchi mzalendo. Dk Shein pia aliahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ), itaendelea kulinda malengo na dhamira ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa faida ya wananchi wake. Alitoa mfano wa tamko la Serikali
la Septemba 23, 1964 alipotangaza elimu bila ya malipo.
Kabla ya
Mapinduzi, kwa mujibu wa Dk Shein, zilikuwepo shule 62 zilizokuwa
zikitoa elimu kwa kubagua wananchi kwa makabila yao, lakini leo zipo
zaidi ya shule 342 za msingi za kizalendo, shule za sekondari 252 na
vyuo vikuu vitatu.
“Ndugu wananchi tumepiga hatua kubwa katika
elimu na bado tunaendelea kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika
elimu...kabla ya Mapinduzi hatukuwa vyuo vikuu, sasa vipo vitatu,”
alisema Shein.
Katika afya, Dk Shein alisema pia wamepiga hatua
kubwa ambapo kwa sasa hakuna mwananchi anayetembea kilometa tano,
kutafuta huduma za afya. Kabla ya Mapinduzi, vilikuwepo vituo vya afya
36 sasa vipo vituo vya afya 134, ambapo sasa mwananchi atatembea chini
ya kilomita 3 kufikia huduma ya afya.
Mbali na kusogeza huduma
za afya karibu na watu, Dk Shein pia alisema maradhi yaliyokuwa
yakitishia afya za wananchi kama malaria, yamepungua na kufikia asilimia
0.3.
Pia, Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), tayari kimeanza kutoa
shahada ya kwanza ya udaktari, ambapo kwa kiasi kikubwa tatizo la
upungufu wa madaktari litakuwa limepata ufumbuzi wake.
“Tumepiga
hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya… yalikuwepo maradhi
yaliyokuwa yakitishia uhai wa wananchi kama malaria kwa kiwango cha
asilimia 45 katika mwaka 1990 na sasa tumeyashusha hadi asilimia 0.3,”
alisema Dk Shein.
Kuhusu uchumi, Dk Shein alisema umeimarika na
kufikia ukuaji wa asilimia saba na lengo ni kufikia ukuaji wa asilimia
7.5 ifikapo mwakani. Pato la kawaida la mwananchi sasa limefikia dola
656, ambapo mfumuko wa bei umepungua kwa kiwango kikubwa baada ya kuwepo
kwa udhibiti ikiwemo bidhaa muhimu za vyakula kupunguzwa kodi ili kutoa
nafuu kwa wananchi.
Awali, Dk Shein aliwataka Wazanzibari
kuendelea kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao ndiyo
kielelezo cha Taifa la Tanzania. Alisema Muungano hivi karibuni,
utafikia umri wa miaka 50 na wananchi wa pande mbili zilizoungana,
wanayo kila sababu ya kusherehekea.
“Wazanzibari Muungano wetu
karibuni utafikia umri wa miaka 50 tangu kuasisiwa kwake na viongozi wa
Taifa hili, kwa hivyo nawaombeni mjitokeze kwa wingi kusherehekea,”
alisema.
Dk Shein alisema Mapinduzi ya Zanzibar, yanakabiliwa na
changamoto mbalimbali na moja ni kutunza mafanikio hayo kwa kudumisha
amani na utulivu. Aliwataka wananchi pamoja na wanasiasa na watu wa
dini, kujenga tabia ya kutii sheria za nchi ili kulinda Mapinduzi ya
Zanzibar.
“Nawaomba wananchi tuige mambo yaliyofanywa na waasisi
wa Mapinduzi ya Zanzibar.....kila mmoja atimize wajibu wake ikiwemo
kufanya kazi kwa bidii na nidhamu na tuepuke kufanya kazi kwa mazoea,”
alisema.
Dk Shein alisema mabadiliko ya kumi ya Katiba ya
Zanzibar ya 2010, yalisababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
ya Zanzibar, ambayo inatokana na maridhiano ya kisiasa. Alisema
Serikali hiyo imepata mafanikio kwa kutekeleza majukumu yake kwa
kuimarisha amani, umoja, na mshikamano wa Taifa.
“Tumeanza
vizuri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo amani na utulivu na
mshikamano vimeimarika kwa nguvu zote,” alisema.
Sherehe hizo
zilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib
Bilali na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Pia, walikuwepo marais wastaafu
akiwemo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu wa ya
Tatu, Benjamin Mkapa.
Mara baada ya Dk Shein kuingia katika
Uwanja wa Amaan akiwa katika gari la wazi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), aliwapungia wananchi mkono na kuwasalimia. Mizinga
21 ilipigwa kwa heshima yake ikiwa ishara ya kumkaribisha pamoja na
kukagua gwaride linaloundwa na vikosi vya JWTZ, Jeshi la Polisi, vikosi
vya SMZ vya Mafunzo, Jeshi la Kulinda Uchumi (JKU), Valantia na KMKM na
Zima Moto.
Wageni waalikwa katika sherehe hizo ni pamoja na Rais
wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alishangiliwa wakati alipoingia
katika Uwanja wa Amaan na kufuatiwa na Rais wa Jamhuri ya Comoro,
Ikililou Dhoinine pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Miji na Vijijini wa
Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Weixin.
Akizungumza katika
sherehe hizo, Rais Museveni aliipongeza Tanzania kwa kusaidia uhuru wa
Uganda, ambapo Jeshi la Tanzania lilishiriki kikamilifu kupambana na
wavamizi. Museveni alizungumza Kiswahili kwa ajili ya kuienzi lugha
hiyo, ya Afrika ya Mashariki na kusisitiza umoja na mshikamano wa
Tanzania pamoja na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.
“Nimeamua
kuzungumza Kiswahili cha Afrika ingawa Kiswahili changu ni kibovu,
lakini bora kuliko kuamua kuzungumza lugha ya wakoloni,” alisema
Museveni huku akishangiliwa na mamia ya watu waliofurika.
Wazanzibari
wanaendelea kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo
utawala wa Sultani wa Oman ulipinduliwa na wazalendo kuchukua hatamu ya
kuongoza dola baada ya kudumu kwa miaka 132.
Jan 13, 2014
RAIS SHEIN ALEZEA MAFANIKIO YA MAPINDUZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment