Jan 7, 2014

Michango Holela Yawakwamisha Watoto Kujiunga Darasa La Kwanza


Mwalimu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kivule ya Manispaa ya Ilala, Wilson Muhemba akionyesha ubao ulioandikwa gharama za uchangiaji wa mtoto anayeingia darasa la kwanza jana. 
 
 
Watoto wengi washindwa kuandikishwa kutokana na kutakiwa kulipa michango mbalimbali.

Msimu wa uandikishaji watoto wanaoanza darasa la kwanza, umeanza, huku kukiwa na malalamiko lukuki hasa kutokana na michango inayotozwa kwa watoto wanaokwenda kuanza darasa la kwanza.
 
Itakumbukwa, Novemba 7, 2012, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Majaliwa Kassim Majaliwa alisema bungeni mjini Dodoma kuwa ni kosa kwa walimu wakuu kutoza fedha kwa watoto wanaoanza darasa la kwanza na atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Majaliwa alisema kama ni michango ni ile iliyokubaliwa na wazazi wenyewe, Kamati za Shule lakini pia na kupata baraka za mamlaka husika za elimu katika Halmashauri au Wilaya.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Serikali, inaonekana kupigwa kumbo huku wazazi wakishangaa michango hiyo, ambayo mingine haieleweki na mingine ilikubalika kupitia kamati za shule.
Tozo la kujiandikisha
Wazazi wa watoto waliokwenda kujiandikisha katika Shule ya Msingi Kivule wameulalamikia uongozi wa shule hiyo kuwachagisha kiasi cha Sh40,000 kwa ajili ya watoto wanaojiunga darasa la kwanza jambo lililosababisha watoto kushindwa kujiunga.
Malalamiko kama hayo ambayo yako kwenye shule mbalimbali, pia yaliibuka katika Shule ya Msingi Mtoni, Dar es Salaam kwa wazazi kulalamikia kutozwa Sh33,500 wakati mjini Morogoro katika Shule ya Msingi Kambarage iliyopo Kata ya Chamwino katika Manispaa ya Morogoro michango ilifikia Sh50,000 kwa kila mzazi.
Katika Shule ya Msingi Kivule, Dar es Salaam, wazazi wameulalamikia uongozi kukataa kuwaandikisha watoto na wazazi kulazimishwa kutoa Sh40,000 ndipo watoto wao waandikishwe kuanza darasa la kwanza mwaka huu.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Wilson Muhemba, alikana madai hayo na kusema anachoelewa yeye ni mchango wa Sh15,000 kwa ajili ya kujenga madarasa ya shule mpya ambayo ilipitishwa kwenye kikao cha wazazi.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha; Rozi Mwing’a alisema alifika shuleni hapo kwa ajili ya kuwaandikisha watoto wake wawili aliambiwa atoe mchango wa Sh40,000 kwa kila mtoto hivyo imesababishia kushindwa kuwaandikisha watoto hao.
Alisema wanachangia michango wa ujenzi wa shule Sh15,000, mchango wa fulana Sh6,000, mchango wa mafunzo ya awali Sh6,000, nembo Sh1,000 na ulinzi ni Sh5,000.
Mwing’a alisema mchango mwingine wa fomu Sh5,000, kupima uzito Sh1,000, picha za pasipoti Sh3000 na mchango wa madaftari saba Sh1,500.

Kwa hisani kubwa ya MWANANCHI.

0 comments:

Post a Comment