Jan 7, 2014

Ikhwanul Muslimin kuishitaki serikali ya Misri huko ICC

Harakati ya Ikhwanul Muslimin inapanga mikakati ya kuifungulia mashtaka serikali ya mpito ya Misri kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), kutokana na jinai zilizofanywa na serikali hiyo dhidi ya binadamu  nchini humo.

John Dugard mmoja wa mawakili wa Ikhwaanul Muslimin amesema kuwa kuna ulazima wa kuutumia utawala wa kijeshi wa Misri ujumbe wa wazi kwamba unakabiliwa na hatari ya kufuatiliwa kisheria.
Dugard ameeleza kuwa, licha ya kuondolewa madarakani Muhammad Morsi, Rais aliyechaguliwa na wananchi wa Misri, jeshi la nchi hiyo limetenda jinai nyingi kama za kufanya mauaji, kuwatesa wananchi na baadhi yao kuwahukumu adhabu za vifungo bila ya hatia.

Wakati huohuo, serikali ya mpito ya Misri imeuomba Umoja wa Afrika kuangalia upya uamuzi wake wa kusimamisha uanachama wa nchi hiyo kwenye umoja huo. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Umoja wa Afrika ulichukua uamuzi huo baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani Muhammad Morsi tarehe 3 Julai mwaka 2013, na badala yake kumuweka madarakani Adly Mansour.

0 comments:

Post a Comment