Jan 15, 2014

Masheikh wasisitiza umoja, amani


Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (kushoto), Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik (kulia), wakiwa kwenye sherehe za Maulid kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam juzi usiku. Picha na Venance Nestory.  



“Ninaomba Waislamu na watu wa dini nyingine kuwa pamoja, tuondoe tofauti zetu kwani sisi Watanzania ni watu tuliozoeleka kwa kuwa na amani, nisingependa kuona dini zetu zinasababisha uvunjifu wa amani.”

Viongozi mbalimbali wa siasa na Kiislamu nchini, wamehimiza amani, umoja, mshikamano wa Watanzania ili kuliepusha taifa na balaa la kupoteza amani.
 

Walisema hayo katika maadhimisho ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyofanyika juzi usiku.

Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliwataka watu wa dini zote kuondoa tofauti zao ili kudumisha amani iliyopo nchini kwa muda mrefu na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba amewataka Waislamu nchini kuepuka migogoro ndani ya misikiti inayoweza kuwagawa.

Mufti

Akihutubia mhadhara wa kitaifa wa Waislamu uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Ujiji, Kigoma, Mufti Simba aliwataka waumini wa dini hiyo kuepuka migogoro ndani ya misikiti inayoweza kuwagawa na kuzusha vurugu miongoni mwao.

Alisema migogoro na vurugu ndani ya misikiti imesababisha Waislamu kukosa nguvu na umoja miongoni mwao na kujikuta wakipoteza fursa ya kupiga hatua za maendeleo kwa kujenga miundombinu ya kijamii kama vile shule, vyuo vikuu na hospitali.

“Ninawaasa Waislamu kuwa makini na baadhi ya watu wanaotaka kutugawa kwa masilahi yao binafsi. 

Tuepuke sana migogoro baina yetu ndani ya misikiti, wale wanaouza viwanja vya misikiti na mali za Waislamu hawana budi kuacha mambo hayo mara moja kwa vile ndiyo kiini cha migogoro mingi.

“Tujifunze kwa wenzetu Wakristo ambao kila wanapopata viwanja, huvitumia kujenga miundo mbinu ya shule, vyuo na hospitali ambazo mwishowe zinatusaidia hata sisi Waislamu kupata maarifa. 

Hapa ndipo tunapotakiwa tujifunze kufanya mema ndani ya jamii zetu kwa faida ya taifa na Waislamu wenzetu.”

Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Jongo aliwataka Waislamu kuacha kulalamika kwamba Serikali inawakandamiza Waislamu na kuwapendelea Wakristo akisema jambo hilo si kweli.

“Waislamu tumekuwa tukilalamika kwamba kuna mfumo-kristo unaofanya kazi ndani ya Serikali na utawala wa nchi yetu. Hizi tuhuma si za kweli na hazipo kabisa. 

Zaidi kinachotugharimu sisi Waislamu ni kuendekeza migogoro baina yetu na kufanya mambo yasiyo ya kistaarabu katika Jamii,” alisema Sheikh Jongo.

Alisema baadhi ya kesi zilizopo mahakamani zilizofunguliwa na Waislamu dhidi ya wenzao ni dalili ya kushuka kwa maadili na hivyo kuwa kichocheo cha kudumaza maendeleo ya Waislamu.

Pia alitaja ugomvi unaotokea ndani ya misikiti kuwa ni miongoni mwa mambo yasiyokubalika katika jamii ya Kiislamu.

 HAPA BAADHI YA WAKAZI WAKIMTAZAMA NGAMIA AMBAYE ALIKUWA NI KIVUTIO KATIKA ZAFFA ILIYOFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM.(PICHA KWA IHSANI KUBWA YA UKHT THUWAIBA)

0 comments:

Post a Comment