Jan 23, 2014

Amnesty Int'l: Misri inakiuka haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limekosoa vikali ukatili wa vikosi vya usalama vya Misri dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani Muhammad Morsi.

Katika ripoti iliyotolewa jana Jumatano kabla ya maadhimisho ya mwaka wa tatu wa mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta Hosni Mubarak, Amnesty imesema watawala wa Misri wanatumia kila njia inayowezekana kuwakandamiza wapinzani na kukiuka haki za binaadamu.  

Mkuu wa Amnesty International Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Hassiba Hadj Sahraou amesema 'Baada ya kupita miaka mitatu, matakwa ya 'Mapinduzi ya Januari 25' ya kutaka kuheshimiwa haki za binaadamu hayajafikiwa. 

Watu kadhaa walioongoza mapinduzi hayo wako korokoroni huku ukandamizaji na ukiukaji sheria ukiwa jambo la kawaida.'

 Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu limeongeza kuwa watu 1,400 wameuawa na vikosi vya usalama katika machafuko ya kisiasa yaliyoanza Julai 3 mwaka jana baada ya jeshi kumuondoa madarakani Morsi. 

Wafuasi wa Morsi wamekuwa wakiandamana mara kwa mara wakitaka arejeshwe madarakani.

0 comments:

Post a Comment