Dec 21, 2013

Mawaziri wango'oka

Mawaziri walioenguliwaMASHAMBULIZI ya wabunge dhidi ya mawaziri wanne kushindwa kusimamia wizara zao, yamemfanya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kuanzia jana.

Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Awali kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hajalieleza Bunge, uamuzi huo wa Rais Jakaya Kikwete, Waziri Kagasheki alitangaza kujiuzulu wadhifa wake baada ya kuguswa na ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyokuwa ikichunguza madhila yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili.

Balozi Kagasheki, ameamua kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutuhumiwa kushindwa kusimamia kikamilifu Operesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa ikifanywa na wizara yake.

Alisema amesikiliza kwa makini sana ripoti ya kamati hiyo na kuamua kuachia wadhifa huo kutokana na madhila yaliyowapata watu, mifugo na mali.

“Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliponiteua alifanya hivyo kwa furaha yake na kuamini nitafanya kazi yake vizuri, yametokea yaliyotokea na yamesemwa mengi… mimi ni mtu mzima nimesoma hisia zenu.

“Nimeamua kujiuzulu wadhifa wangu na nitafuata taratibu zote zinazotakiwa… nitaitaarifu mamlaka ya juu uamuzi wangu,” alisema.

Mara baada ya Kagasheki kutoa taarifa yake hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo, alipopata fursa ya kuzungumza, alisema anaona anaonewa kuhusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na askari waliokuwa kwenye operesheni hiyo.

Aliongeza kuwa kutajwa kwake katika ripoti hiyo kunaonyesha watu walikuwa wana dhamira mbaya dhidi yake.

“Jana usiku nilisoma sana Biblia ambayo ni Zaburi ya 72… nilisali sana jana usiku kwa kuwa niliona dalili za kuonewa, nawaambia matatizo mengi yaliyozunguzwa hayakuwa chini ya wizara yangu.

“Kuna wabunge wamesema wazi wazi hapa kuwa ninaonewa kuingizwa katika mkumbo wa mawaziri wanaotakiwa wawajibike, naapa mbele ya mwenyezi Mungu Subhana wa taala atawalipa wale walioona ninaonewa kwani nilijua hili,” alisema.

Mara baada ya Mathayo kuzungumza, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipewa fursa ya kuzungumza ambapo alisema amezungumza na Rais Kikwete ambaye yupo nchini Marekani juu ya jambo hilo na aliungana na wabunge waliokuwa wakitaka mawaziri hao wawajibike.

Alibainisha kuwa Rais Kikwete pia alitaka kuundwa kwa tume ya kuchunguza madhila yote yaliyotajwa kwenye ripoti ya kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo.

“Nilipomueleza mambo hayo akasema ametengua uteuzi wake kwa mawaziri wote wanne, atakuja kuangalia hapo baadae kwa picha iliyojitokeza. Rais kaona uzito wa tukio hilo, hivyo kaamua kutengua uteuzi wao.

“Tumekubaliana na Rais Kikwete ambaye sasa yupo safarini, akirudi tutakuja kumalizia mambo yaliyobakia… mawaziri hawa wamejiuzulu si kwamba walikuwapo kwenye meneo ya tukio au walishiriki bali vyombo vilivyofanya hivyo vipo chini yao,” alisema.

Pinda alisema pia alizungumza na mawaziri hao juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwao na wabunge pamoja na kamati iliyoundwa na kuchunguza sakata hilo.

“Nilizungumza nao kwa jambo hilo, niliwaambia wabunge wamesema sana, niliwambia kwa kuwa wao ni watu wazima wapime mambo hayo, waheshimiwa hawa wote wamekubali kujiuzulu, wamekubali kujiuzulu kwa sababu mambo hayo yamefanyika chini ya utawala wao,” alisema.

Mara baada ya Pinda kuzungumza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, alisema hatua ya kujiuzulu na ripoti hiyo inafungua milango ya sheria kuchukua mkondo wake kwa wale wote waliohusika.

“Pia tunaomba Bunge liridhie uundaji wa tume ya uchunguzi wa kimahakama ambayo tuna hakika itayaangalia mambo yote yaliyotokea kwa kina zaidi,” alisema.

0 comments:

Post a Comment