Dec 14, 2013

Jeshi la Misri lawashambulia waandamanaji


Vikosi vya usalama nchini Misri vimewashambulia waandamanaji katika miji mbalimbali ya nchi hiyo waliokuwa wakiandamana kudai utawala wa sheria. 

 Baadhi ya miji iliyoshuhudia vikosi vya usalama vikiwashambulia waandamanaji ni mji mkuu Cairo na Port Said.

Baada ya Sala ya Ijumaa, miji mbalimbali ya Misri leo ilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wanaotaka kurejeshwa utawala wa sheria nchini humo.
Vikosi vya usalama vilitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya maelfu ya waandamanaji katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. 

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali wakisisitiza upinzani wao dhidi ya wanajeshi wanaotawala nchini humo waliomuondoa madarakani Rais halali wa nchi hiyo Muhammad Mursi.

 Maandamani hayo yaliandaliwa na wanachuo ambao ni wafuasi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimiin. 

Habari nyingine kutoka Misri zinasema kuwa, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo imekaribisha kwa mikono miwili uamuzi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kusimamia kura ya maoni ya Katiba. 

Kamisheni Kuu ya Uchaguzi ya Misri kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais zimeamua kwamba, kura ya maoni kwa ajili ya Katiba mpya ifanyike tarehe 11,12 na 13 mwezi Januari mwaka ujao wa 2014.

0 comments:

Post a Comment