Nov 1, 2013

Serikali Yapunguza Alama Za Ufaulu




Hatimaye Serikali imepunguza alama za ufaulu kwa mtihani huo pamoja na ule wa Kidato cha Sita.
 

Aidha serikali imetangaza kuwa, mtihani wa taifa wa kidato cha nne na sita utakuwa na alama 60 za ufaulu, huku alama 40 zilizobaki zitatokana na zile za maendeleo ya mwanafunzi shuleni (CA).

Katika mfumo huo mpya, wizara hiyo pia imefuta daraja la sifuri na badala yake kutakuwa na daraja la tano.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alipotangaza uamuzi huo wa Serikali jana na kueleza utekelezaji wa utaratibu huo utaanza kwenye mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka huu.

“Hatua hii imechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza kuanzia mwaka 2011. Tangu wakati huo kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika,” alisema Profesa Mchome.

Alisema kuwa, alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) katika kupanga matokeo hayo, kwa kidato cha nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F= 0-34 kwa upande wa kidato cha sita A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.

Alisema mfumo mpya, umehusisha alama za kidato cha nne na cha sita na kuwa kuanzia sasa A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19.

“Alama A itakuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ itakuwa ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha kabisa,” alisema Profesa Mchome.

Alisema pia kuwa, wamebadilisha mfumo wa madaraja ambao awali kulikuwa na daraja la kwanza, la pili, la tatu, la nne na sifuri.

“Lile la sifuri tumeliondoa, badala yake kutakuwa na daraja la tano, lengo ni kuweka mlolongo mzuri zaidi,” alisema.

Alisema, alama hizo zitakuwa ni mgando (fixed grade range).

Profesa Mchome alisema kuwa, utaratibu wa sasa wa kupanga matokeo hayo kwa madaraja, utabadilika muda wowote kuanzia sasa na kwamba utakaokuwa ukitumika ni ule wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Point Average ‘GPA’).

0 comments:

Post a Comment