Nov 8, 2013

Hatuna Mpango Kujitoa EAC-KIKWETE


 


RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania haina mpango wa kujitoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), itaendelea kuwepo licha ya kutengwa na baadhi ya nchi wanachama.

EAC inahusisha nchi tano washirika za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania ambapo kwa siku za karibuni wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya wanaonekana kuanzisha umoja wao ndani ya jumuiya hiyo.

Alisema anaamini kinachoifanya Tanzania ichukiwe na nchi nyingine wanachama wa EAC ni msimamo wa viongozi wake kuhusu ardhi, ajira, uhamiaji na uharakishwaji wa shirikisho.

Akilihutubia Bunge mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema hataki mambo yaliyotokea mwaka 1977 yajirudie huku akisisitiza kwamba Tanzania itaendelea kuwepo kwenye jumuiya hiyo.

Alisema Tanzania inatimiza ipasavyo wajibu wake kwa jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya EAC huku akisisitiza kwamba sababu ya wakuu wa nchi hizo tatu kufanya mambo yasiyohusu jumuiya haieleweki.

“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.

“Tanzania haijafanya lolote baya dhidi ya jumuiya hiyo au kwa nchi mwanachama kama kuna ushahidi uletwe… tusingekuwa na sababu ya kuchangia dola milioni 12 za Marekani kila mwaka, hii ni fedha nyingi,” alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wenzake hao walifanya mikutano mitatu, yaani Juni 24 hadi 25 mwaka huu, mjini Entebbe-Uganda, mkutano mwingine walifanya mjini Mombasa-Kenya Agosti 28  na Oktoba 28 walikutana tena mjini Kigali, Rwanda.

“Wanafanya mikutano hiyo bila kutualika… wanazungumzia masuala ya jumuiya, nimeambiwa eti huo ni ushirikiano kwa walio tayari, wanasema tumekuwa kikwazo tunawachelewesha wenzetu kwenye maendeleo.

“Maneno haya yamekuwa yakijirudia lakini hayana ukweli wowote, sababu zao hazina mashiko,” alisema Rais Kikwete huku akisisitiza kwamba Tanzania ni mwanachama mtiifu, mwaminifu na mvumilivu kwa jumuiya.

Msimamo wa EAC unaelekeza kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali.

Alisema kitu cha kushangaza ni pale nchi hizo tatu zinapofanya mambo yaliyoamuliwa ndani ya EAC, ambayo lazima nchi washirika wakubaliane.

Rais Kikwete aliyataja mambo manane yaliyoamuliwa na wakuu wa nchi za Uganda, Kenya na Rwanda kuwa ni kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala,  Kigali  na Bujumbura, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.

Jambo jingine ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Uganda na Sudan ya Kusini, kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, kuanzisha himaya moja ya ushuru wa forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakuu wa nchi hizo pia wamekubaliana kuharakisha Shirikisho la EAC na kwamba itaundwa kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho, kuharakisha uanzishwaji wa viza ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao.

Alisema mambo hayo yanachanganya yale ya jumuiya na yasiyokuwa, huku akiyataja mambo manne ya EAC yaliyopo kwenye mipango ya viongozi wa nchi hizo ‘zinazoisaliti’ jumuiya.

“Hata hivyo bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama kuamua…lakini, hivi ndugu zetu hawa wanaona muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?

“Nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoreti hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa kaskazini magharibi mwa Tanzania.

“Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo ambalo wenzetu wanalizungumzia,” alisema.

Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa–Kampala – Kigali – Bujumbura alisema halina tatizo kwa kuwa si mradi wa EAC, upo chini ya mamlaka ya nchi wanachama.

Hata hivyo, alisema ni vema kutambua kuwa ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara, usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za EAC ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na jumuiya hiyo.

Alisema jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana kuna ‘East African Railway Masterplan, inayohusisha East African Road Network na Lake Victoria Development Programme kwa Ziwa Victoria.

“Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi… kimetokea nini tangu tukutane wakuu wa nchi zote za Jumuiya Arusha Aprili 28 na vikao vyao vilivyoanza Juni 24 walipoamua kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana. Haijawahi kuwa hivi kabla,” alisema.

Alisema uchumi imara ndiyo kichocheo cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa jumuiya yetu.

Rais aliongeza kuwa kabla ya kuanza tena kwa EAC asilimia 78.4 ya Watanzania waliohojiwa na kamati iliyoongozwa na Profesa Samwel Wangwe waliunga mkono kuwepo kwa shirikisho huku asilimia 25.4 kati yao wakitaka uharakishwaji wake.

0 comments:

Post a Comment