Oct 22, 2013

Wafuasi wa Sheikh Ponda HURU


 


Penye ukweli uongo hujitenga,hayo yamedhihiri jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,baada ya kuwaachia huru wafuasi 52 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokuwa wakitumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela.
Wafuasi hao wa Ponda waliachiwa huru jana baada ya Mahakama Kuu kutengua adhabu ya kifungo hicho waliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wafungwa hao walihukumiwa kifungo hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Machi 21, 2013 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama kutenda makosa, kukaidi amri ya Polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na Polisi, kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa wakili wao, Mohamed Tibanyendela walikata rufaa Mahakama Kuu, wakiwasilisha sababu tisa za kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu, iliyowatia hatiani pamoja na adhabu yake.
Katika hukumu yake jana, Jaji Salvatory Bongole licha ya kukubaliana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu kuwa washtakiwa walikuwa na hatia, lakini alikubaliana na hoja za wakili wao Mohamed Tibanyendela kuwa adhabu waliyopewa haikuwa sahihi kulingana na makosa yaliyowatia hatiani.
Katika shtaka la pili, warufani walitiwa hatiani kwa kosa la kufanya mikusanyiko haramu na shtaka la tatuwalitiwa hatiani kwa kosa la kukaidi amri halali ya Jeshi la Polisi.
Jaji Bongole alisema kwamba katika makosa hayo warufani walishtakiwa chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa kwa mujibu wa Miongozo ya Jeshi la Polisi (Police General Oders-PGO), warufani hao walipaswa kuhukumiwa adhabu ya faini ya Sh50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela na si mwaka mmoja.
“Hivyo ninakubaliana na hoja za wakili wa warufani kuwa utetezi wa kupunguziwa adhabu haukuzingatiwa wakati wa kuadhibiwa na ninatengua adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja na kuibadilisha kuwa kifungo cha miezi mitatu jela,” alisema Jaji Bongole na kuongeza:
“Warufani walihukumiwa adhabu hiyo Machi 21, 2013 na leo ni Oktoba 21, 2013. Kutoka Machi 21 hadi Oktoba 21, 2013 wameshakaa jela zaidi ya miezi mitatu, basi wameshamaliza kifungo chao.”
Pia Jaji Bongole alikubaliana na hoja za Wakili Tibanyendela kuwa Hakimu wa Mahakama ya Kisutu Fundi Fimbo alikosea kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama na kuwaadhibu kwa kosa hilo wakati tayari alikwishawatia hatiani kwa kosa la kufanya mikusanyiko isiyo halali.

Aidha mwishoni mwa wiki iliyopita waislamu wangine waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia katika kesi ikiyo wakabili ya kuchoma moto makanisa mwishoni mwa mwaka jana.

0 comments:

Post a Comment