Sep 9, 2013

WANAFUNZI WALIPUKIWA NA BOMU

WANAFUNZI wawili wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Matombo katika Wilaya ya Morogoro, wamejeruhiwa na wengine watatu kunusurika, baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu wakati wakitoka shuleni baada ya mmoja wao kukigonga na muwa aliokuwa anakula.
Wanafunzi hao waliojeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao ni Lucien Juma (14) na Anthonia Charles (15), ambao ni wakazi wa Kijiji cha Konde, Tarafa ya Matombo wilayani Morogoro.

Lucien aliyelazwa wodi namba moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu, alisema walipatwa na tukio hilo wakati wakitokea shuleni, ambapo njiani walikutana na kitu mfano wa balbu ya tochi ambacho hata asubuhi wakati wanakwenda shule walikiona na kukipuuza.

Alisema wakiwa kundi la watu watano njiani kutoka shuleni, walikikuta tena kitu hicho ambapo mmoja wa wanafunzi aliyekuwa anakula muwa alikirushia kitu hicho ganda la muwa na kulipuka na kutoa mshindo mkubwa uliosikika hadi maeneo ya mbali.

Kwa upande wake, Dk. Francis Semwene, anayemtibu Lucien katika wodi namba moja alikolazwa, alisema majeruhi huyo anaendelea vizuri na amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo sehemu za siri, paja na sehemu ya nyonga na katika maeneo hayo walifanikiwa kutoa vitu mfano wa vyuma vidogo vidogo.

Naye, babu wa mwanafunzi Lucien, Ekaristi Martini, alisema walipata taarifa za tukio hilo wakiwa shamba wanaendelea na kilimo na baada ya kufika eneo la tukio, walikuta wasamaria wema wamewasaidia watoto hao na kuwapeleka Hospitali ya Misheni ya Matombo ambapo walipatiwa huduma ya kwanza na kupewa rufaa kuja hospitali hiyo ya mkoa kwa matibabu zaidi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, John Laswai, alithibitisha kujeruhiwa kwa wanafunzi hao, ambapo majeruhi Anthonia aliyejeruhiwa sehemu ya makalio alitibiwa na kuruhusiwa na wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini kitu kilichowajeruhi wanafunzi hao kama kilikuwa ni bomu ama vinginevyo.