Sep 20, 2013

Walimu Punguzeni Bakora

KUMCHAPA mwanafunzi kunaweza kumsababishia usugu utakaomfanya asijali jambo lolote baya analokatazwa kwa kuwa atakuwa amezoea kuchapwa. Watoto wa siku hizi wamekuwa na uelewa mkubwa wa mambo ukilinganisha na wa zamani. Unaweza kukuta watoto wakimaliza shule ya msingi wakiwa wadogo hivyo huingia sekondari wakiwa bado hawajakomaa. Hivyo, ili kuepuka matatizo ya hapa na pale, adhabu wanazopewa ni muhimu ziendane na umri wao.
Mwalimu anao uwezo wa kumrekebisha mwanafunzi hata kwa maneno tu. 

Adhabu ya viboko kwa namna moja au nyingine si nzuri kwa watoto kwa kuwa inaweza kusababisha madhara makubwa. Kama mwanafunzi ni mkaidi kupita kiasi ni vema akapewa adhabu ndogondogo kama kufanya usafi katika uwanja wa shule, darasani bila msaada wa wenzie, kufyeka nyasi, kufagia na nyingine nyingi za aina hiyo.

Adhabu ya viboko humfanya mtoto kutokuwa mdadisi wa mambo. Humfanya ashindwe kuwa karibu na mwalimu kwa kuhofia kuchapwa.

Hivi majuzi, shule moja mkoani Iringa Wilaya ya Makambako, mtoto wa darasa la tatu baada ya kukosea kuandika herufi, mwalimu wake aliamua kumpiga katika tezi za shingo na mgongoni kwa kutumia rula ya kupigia mstari ubaoni. Baada ya kumpiga mwanafunzi huyo alifariki. Alipopelekwa hospitali ikabainika chanzo cha kifo chake ni kipigo kutoka kwa mwalimu. Alibainika akiwa na usaha na damu ilivilia katika ubongo wake.

Jambo kama hili linapotokea, mzazi huwa katika wakati mgumu.

Sasa basi, kwa kuwa Serikali imeruhusu viboko kwa wanafunzi na ukizingatia kuwa kila binadamu ana kiwango chake cha hasira, suala hili linaweza kuleta hasara kubwa kwa wazazi kupoteza watoto wao hasa ukizingatia siku hizi maradhi ni mengi.

Katika hali ya kawaida, ni rahisi mno kwa wazazi kujenga uhasama na walimu kutokana na vipigo wanavyopata watoto wao.

Baadhi ya waalimu wamekua wakichapa watoto bila hata kuangalia ni eneo gani analomchapa mwanafunzi. 

Tumeshashuhudia wanafunzi wakitokwa na damu puani kutokana na kipigo wanachopata kutoka kwa walimu. Suala kama hili ni hatari kwa wanafunzi kwani athari zake ni kubwa kuliko kumfundisha mwanafunzi kuwa na maadili mema shuleni na hata nyumbani.

Ikiwezekana Serikali iangalie upya suala hili maana kuna watoto wanapata ulemavu kutokana na viboko shuleni. Mkoani Iringa kuna mwanafunzi hadi leo hii hawezi kutembea wala kujisogeza kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na kuchapwa viboko visivyo na idadi tena bila utaratibu na mwalimu wake.

Mtoto si nyoka hadi apigwe kichwani, haijalishi ametenda kosa gani. Hivyo walimu wasijisahau pindi wanapowachapa watoto wa wenzao kwa kuwa nao pia ni wazazi.

Tunafahamu kuwa viboko shuleni vinasaidia kurekebisha wanafunzi hasa wale watukutu. Lakini jambo la msingi walimu wanapaswa kuwachapa kwa utaratibu na wawe na kiwango maalumu cha fimbo anachostahili kuchapwa mtoto kulingana na kosa alilofanya, pia kuangalia umri wake kwani wengine huanza masomo wakiwa na umri mdogo mno.

Walimu wanapaswa kuwa makini katika hili ili kuepuka lawama, vifo shuleni na uhasama baina yao na wazazi

0 comments:

Post a Comment