Wizara ya Afya Zanzibar imeruhusu mshtakiwa wa nne,
Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam
(Jumiki), Sheikh Azzan Khalid Hamdani (56), kupelekwa nje kutibiwa baada
ya kukosekana tiba ya maradhi yanayomsumbua visiwani hapa.
Sheikh Azzan alilazwa Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja kuanzia
Septemba Mosi, mwaka huu baada ya kupoteza nguvu akiwa Gereza la Kiinua
Miguu na imebainika anasumbuliwa na vijiwe kwenye figo.
Kuruhusiwa kwa Sheikh Azzan kupata tiba nje, kumethibitishwa na
wakili wake, Salum Towfiq mbele ya Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu
Zanzibar, Yesaya Kayange.
Wakili Towfiq alisema mteja wake hali yake siyo nzuri, amepata barua
ya Wizara ya Afya Zanzibar kwamba maradhi yanayomsumbua hayatibiki
Zanzibar na kutaka mwongozo.
Licha ya ombi hilo, Wakili Tawfiq aliwasilisha malalamiko kuwa wateja
wake wananyanyaswa, ikiwamo kutopata nafasi ya kuwasiliana na familia
zao kupitia simu na wanapokuwa kwenye mazingira ya Mahakama.
Alidai Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kimewawekea utaratibu wa
kukutana na familia zao mara mbili kwa mwezi, huku akiomba Mahakama itoe
mwongozo.
Pia, alidai hata wanafamilia wanapotaka kwenda mahakamani kusikiliza
mwenendo wa kesi hukumbana na misukosuko na kushindwa kuingia ukumbini
kutokana na kuimarishwa ulinzi na kuzuia njia za kuingia na kutoka.
0 comments:
Post a Comment